1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi waukomboa mji wa Kunduz

Admin.WagnerD1 Oktoba 2015

Maafisa wa Afghanistan wamesema sehemu kubwa ya mji wa Kundus imeshakombolewa na siku tatu baada ya mji huo kutekwa na wapiganaji wa Taliban. Hata hivyo taarifa za kijeshi zinasema mapigano bado yanaendelea.

https://p.dw.com/p/1Ggog
Picha: picture-alliance/AP Photo/STR

Majeshi ya serikali ya Afghanistan yameonekana katika mji wa Kundus wa jimbo la kaskazini mwa Afghanistan siku tatu baada ya majeshi hayo kupokonywa udhibiti wa mji huo kadhia iliyozingatiwa kuwa aibu kwa majeshi ya serikali na washirika wao wa Marekani. Lakini kwa mujibu wa taarifa,misafara ya magari ya majeshi ya Afghanistan leo iliweza kuingia katika sehemu ya kati ya mji wa Kunduz baada ya kuanzisha mashambulio ya kuurudisha mji huo katika udhibiti wa majeshi ya serikali.

Majeshi ya Afghanistan yalisaidiwa na vikosi maalumu vya mfungamano wa kijeshi wa NATO. Wakaazi wa mji huo waliliambia shirika la habari la AFP kwamba mapambano ya bunduki bado yalikuwa yanasikika katika sehemu za mji wa Kunduz na kwamba maiti za wapiganaji wa Taliban zimetapakaa katika mitaa ya mji huo. Pia wamearifu kuyaona magari yalioungua na kuharibika

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ameeleza kwamba majeshi ya usalama yanaudhibiti mji wa Kunduz lakini amesema itachukua muda mrefu kuwafagilia mbali wapiganaji wa Taliban kwa sababu wanajificha miongoni mwa raia na kushambulia.

Mkaazi mmoja wa mji wa Kunduz ameitaka serikali ya Afghanistan iurudishe mji wa Kunduzu katika udhibiti wake.Amesema wanaitaka serikali ihakikishe ulinzi wa mji wa Kunduz. Ametamka kwamba wao hawana jingine wanalolitaka kutoka serikalini ila usalama wa mji wa Kunduz.

Mji wa kunduz baada ya majeshi ya serikali kuingia
Mji wa kunduz baada ya majeshi ya serikali kuingiaPicha: Reuters

Hata hivyo msemaji wa Taliban amedai kwamba wapiganaji hao bado wanaendelea na mapambano. Kamanda wao amesema wapiganaji wao wanarudi nyuma na kuondoka Kunduz kama sehemu ya mbinu za kijeshi.

Taarifa zinasema wakaazi wa Kunduz waliokuwa na furaha walijitokeza mapema leo baada ya kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Wakaazi hao waliyashukuru majeshi ya serikali.

Mkurugenzi wa hospitali kuu ya jimbo Saad Mukhtar amefahamisha kwamba mpaka sasa wamezipokea maiti karibu 50 na watu 330 waliojeruhiwa. Mkaazi mwengine wa mji wa Kunduz amedai kwamba wapiganaji wa Taliban walipata kipigo kikubwa jana usiku.

Maafisa wa usalama wamefahamisha kwamba wapiganaji wa Taliban walijipenyeza katika mji wa Kunduz wakati wa siku kuu za Eid.Wapiganaji wa Taliban walifanya uvamizi katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu Rais Ashraf Ghani aingie madarakani nchini Afghanistan.

Mwandishi:Mtullya Abdu. afp,

Mhariri:Gakuba Daniel