1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majejshi ya Syria yakomboa maeneo yote ya Aleppo

Zainab Aziz
8 Desemba 2016

Waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria wamesema, Waasi waliondoka kutoka kwenye mji huo mkongwe baada ya majeshi ya serikali kuendelea kusonga mbele usiku kucha

https://p.dw.com/p/2Tsph
Syrien syrische Armee in Aleppo
Picha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria, waasi waliyaacha maeneo ya mwisho ya mji huo mkongwe baada ya wanajeshi wa serikali kuwazidi nguvu na kuvitwaa vitongoji viwili vya Bab al-Hadid na Aqyul.  waangalizi hao wa haki za binadamu wameeleza kwamba majeshi ya Syria yameendelea kupata ushindi tangu operesheni ya kuukomboa mji wa Aleppo ilipoanza.  Jana usiku vikosi hivyo vya serikali vilishambulia eneo la Al-Zabdiya pamoja na maeneo mengine yanayoshikiliwa na waasi huko Kusini-Mashariki ya mji wa Aleppo.  Takriban watu 15 wameuwawa akiwemo mtoto mmoja kutokana na zoezi hilo la vikosi vya serikali la kuukomboa mji wa Aleppo.  Kwingineko watu 11 wameuwawa miongoni mwao wakiwa watoto 3, hayo ni baada ya waasi kufanya mashambulio dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na serikali.

Kanali mmoja wa jeshi la Urusi amefariki dunia baada kuumizwa vibaya katika mashambulio yaliyofanywa na waasi katika mji wa Aleppo.  Kanali Galitsky amefariki katika hospitali ya kijeshi ambako madaktari walijaribu kuyaokoa maisha yake kwa siku kadhaa.  Urusi pia imetoa taarifa ya kuuwawa kwa wanajeshi wake wawili wa kike baada ya eneo iliyokuwepo hospitali ya jeshi kushambuliwa na waasi katika mji wa Aleppo.

Syrien Präsident Bashar Assad
Rais Bashar al-Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Mashambulio nchini Syria yanaendelea wakati ambapo Urusi  na Marekani zinaendelea kulaumiana  juu ya kuzorota kwa juhudi za kumaliza mapigano katika mji huo wa Aleppo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema kwamba atajaribu kuyafufua mazungumzo ya amani ya Syria baina ya nchi yake na Urusi, mazungumzo hayo yanatarajiwa kuanza tena hapo kesho mjini Hamburg, Ujerumani.  Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema kuwa anatarajia kukutana na Kerry leo au kesho mjini Geneva ili kuanza mikakati ya kuondolewa vikundi vya waasi kutoka katika mji wa Aleppo kabla ya zoezi la kusitisha mapigano halijaanza, Lavrov ameilaumu serikali ya Marekani kwa kurudisha nyuma juhudi za kuleta amani nchini Syria kwa kuwaunga mkono waasi wanaompinga mshirika wake rais Bashar al-Assad.  Lavrov amesema anaona kama mazungumzo ya kutafuta amani nchini Syria baina ya Moscow na Washington hayeleti tija.  

Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema, kuwa ni aibu kubwa kwa jamii ya kimataifa kushindwa kuwaondolea mateso watu wa Aleppo Mashariki.

Mwandishi Zainab Aziz/AFPE

Mhariri:    Yusuf Saumu