1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Ufaransa na Mali yapongezwa

Kabogo Grace Patricla3 Februari 2013

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema kuwa majeshi ya nchi yake yatabakia nchini Mali kwa muda mrefu iwapo yatahitajika kuendelea kupambana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/17XCZ
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande
Rais wa Ufaransa, Francois HollandePicha: Reuters

Akizungumza kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako, hapo jana (02.02.2013), Rais Hollande alisema ugaidi umerudishwa nyuma, lakini bado haujatokomezwa kabisa. Wakati majeshi ya Ufaransa na Mali yakiendelea na jitihada za kuukomboa mji wa Kidal, ngome ya mwisho ya waasi waliolitawala eneo la kaskazini mwa miezi 10 kabla ya majeshi ya Ufaransa hayajaivamia nchi hiyo kijeshi, Rais Hollande amewaambia wananchi wa Mali kwamba ni muda kwa Waafrika kuongoza operesheni za kijeshi, lakini Ufaransa haitawatenga na kuwaacha peke yao.

Amesema Ufaransa itakuwa bega kwa bega na Mali kwa muda wote unaohitajika hadi hapo Waafrika watakapoweza wenyewe kuongoza operesheni za kijeshi. Akiwa mjini Timbuktu, alikopokewa kama shujaa, Rais Hollande aliwashukuru wanajeshi wa Ufaransa na Mali kwa juhudi zao za kuwaondoa waasi kaskazini mwa Mali, ingawa amekumbusha kuwa operesheni hiyo ya kijeshi bado haijamalizika.

Rais wa Mali amshukuru Hollande

Rais wa mpito wa Mali, Diancounda Traore, amemshukuru Rais Hollande kutokana na ufanisi wa wanajeshi wa Ufaransa, ambao amesema umelifanya eneo la kaskazini kukombolewa na kuwa huru. Mbali na Rais Traore kumshukuru Rais Hollande, wakaazi wa mji huo pia wamemshukuru kiongozi huyo wa Ufaransa na kuahidi kumshukuru milele ingawa wamemkumbusha kuwa amefanikiwa kuukata mti, lakini bado ana jukumu la kuondoa kabisa mizizi ya mti huo.

Rais Francois Hollande na Rais Diancounda Traore
Rais Francois Hollande na Rais Diancounda TraorePicha: Reuters

Marais hao wawili walizuru pia katika msikiti wa Djingareybar mjini Timbuktu uliojengwa kwa udongo miaka 700 iliyopita pamoja na maktaba ya Ahmed Baba kwa ajili ya mambo ya kale.

Aidha, walipozuru makaburi mawili ya maimamu ambayo waasi hao waliyaharibu mwezi Julai mwaka uliopita kwa madai kwamba wanaabudu sanamu, Rais Hollande amewaambia maimamu wa msikiti huo kuna haja ya kuuteketeza kabisa kwa sababu hakuna kitu kilichobakia. ''Tutayajenga tena mheshimiwa rais,'', alisema Irina Bokova, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Wakati rais huyo wa Ufaransa yuko Timbuktu, majeshi ya Ufaransa na Mali yalipambana na waasi. Afisa mmoja wa jeshi la Mali ameyasema hayo na kuongeza kuwa waasi waliitumia fursa hiyo kufanya mashambulizi yao, wakitarajia kwamba wanajeshi wangelikuwa wameshughulika zaidi na kuwasili kwa Rais Hollande.

Ufaransa na nia ya kukabidhi operesheni za kijeshi

Huku waasi wakiwa wamefurushwa kutoka miji yote mikubwa isipokuwa Kidal uliopo kaskazini mashariki, Ufaransa ina nia ya kukabidhi operesheni za kijeshi kwa karibu wanajeshi 8,000 wa Afrika ambao wanawasili taratibu nchini Mali na walioidhinishwa na Umoja wa Mataifa.

Lakini kuna wasiwasi kuwa Mali inahitaji msaada wa muda mrefu na huku makundi ya haki za binaadamu yakiripoti mauji yaliyofanywa na wanajeshi wa Mali pamoja na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu.

Wanajeshi wa Mali
Wanajeshi wa MaliPicha: Reuters

Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa wanajeshi wa Mali wamewauwa kwa kuwapiga risasi watu wapatao 13 wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa waasi wenye itikadi kali za Kiislamu katika mji wa Sevare na kuitupa miili yao kwenye visima.

Baadhi ya waliokumbwa na mkasa huo kabla ya majeshi ya Ufaransa hayaijavamia Mali kijeshi, ni watu wa jamii wa Kituareg na Kiarabu. Kutokana na kuongezeka wasiwasi wa kuzuka mashambulizi zaidi, watu wa jamii hizo wamekimbia katika eneo hilo la kaskazini.

Mzozo wa Mali umesababisha watu 377,000 kuyakimbia makaazi yao, wakiwemo 150,000 ambao wameomba hifadhi ya ukimbizi katika mipaka ya Mali. Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Rais Hollande amewatolea wito wanajeshi wa Mali kuheshimu na kuzingatia haki za binaadamu, wito ulioungwa mkono na Rais Traore ambaye pia ameahidi kuongoza mchakato wa maridhiano ya kitaifa na kurejea msimamo wake kwamba anataka kuitisha uchaguzi ifikapo Julai 31, mwaka huu.

Traore aipongeza timu ya mpira wa miguu ya Mali

Ama kwa upande mwingine, Rais wa mpito wa Mali, Diancounda Traore ameipongeza timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Mali baada ya kupata ushindi wa mabao matatu kwa moja ikiwa ni mikwaju ya penalti dhidi ya Afrika Kusini katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika-AFCON 2013, inayoendelea nchini Afrika Kusini.

Timu ya taifa ya soka ya Mali
Timu ya taifa ya soka ya MaliPicha: gettyimages/AFP

Timu hizo zililazimika kupigiana penalti baada ya mchezo kumalizika zikiwa zimetoka sare ya kufungana bao moja kwa moja. Amesema ushindi wa timu ya Mali kuingia nusu fainali, ambao ni ushindi wa kwanza tangu mwaka 1972 ni hatua ambayo imeongeza thamani na ufahari wa Mali, licha ya nchi hiyo kuwa katika mzozo. Amesema ushindi huo utaisaidia Mali kurejea tena katika amani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef