1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maji Tele,Lakini Ni Salama kuyanywa?

P.Martin26 Aprili 2008

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,msimu wa mvua huanza mwezi Aprili katika majimbo ya mashariki yaliobobea maji.Ingawa nchi hiyo hupata mvua kubwa na kuna mito mingi pia,ni shida kupata maji safi.

https://p.dw.com/p/DozA
**FILE** President Joseph Kabila smiles during a meeting with former heads of state in Kinshasa, Congo in this Saturday, Nov. 4, 2006 file photo. Kabila appeared to have an insurmountable lead Tuesday, Nov. 14, 2006, in Congo's runoff election with nearly all the votes counted. (AP Photo/Schalk van Zuydam, FILE)
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: AP

Kwa mujibu wa uchunguzi wa mwisho wa jamii na afya uliofanywa mwaka 2001 na Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,asilimia 46 ya wananchi ndio huweza kupata maji safi.Na vijijini asilimia 60 ya umma hupata maji katika chemchemi lakini nyingi zimechafuka-kama asilimi 30 ya chemchemi ndio zimefanyiwa mpango wa kuzuia uchafuzi wa maji.

Hata katika mji mkuu Kinshasa ulio na takriban watu milioni nane,hakuna mfumo wa kusafisha maji machafu.Idadi kubwa ya vifo nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo husababishwa na magonjwa ya kuambikiza,utapiamlo na hali zinazohusika na uzazi.Mara nyingi magonjwa hayo ya kuambukiza hutokana na maji yaliyochafuka.Hiyo imethibitishwa katika ripoti iliyotolewa mapema mwaka huu na Jumuiya ya Msalaba Mwekundu na Burnet Institute-taasisi inayofanya utafiti wa tiba na afya katika jamii.Naibu mratibu wa UNICEF nchini Kongo,Steven Lauwerier anasema,magonjwa mengi nchini humo yanahusika na masuala kama vile usafi wa maji,iwapo maji yanahitaji kuchemshwa au la na hali ya usafi katika mazingira ya nyumbani.

Kutoka Malengo manane ya Maendeleo ya Milenia yalioyokubaliwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2000, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itaweza kutimiza lengo moja tu utakapofika muda uliowekwa yaani mwaka 2015.Lengo hilo ni kuhifadhi mazingira na kuhakikisha kunapatikana maji safi ya kunywa.Kwa hivyo UNICEF ikishirikiana na serikali ya Rais Joseph Kabila,imeanzisha mradi uitwao "Kijiji cha Afya".

Lengo si kuendeleza mipango ya kupata maji safi tu bali kushughulikia pia mifumo ya afya na usafi.Kwani miradi ikilenga kupata maji safi tu na hali watu hawakoshi mikono yao vizuri basi itakuwa shida sana kupunguza magonjwa kama vile tumbo la kuhara.Kuambatana na mradi wa "Kijiji cha Afya" jamii huomba kushiriki katika mpango huo na baadae kwa msaada wa serikali na mashirika ya kigeni, jamii hiyo hujitahidi kutekeleza malengo kadhaa.Kwa mfano asilimia 80 ya nyumba ziwe na vyoo vinavyofaa na asilimia 70 ya umma katika jamii hiyo uweze kupata maji safi ya kunywa.

Katika mradi mwingine,shirika lisilo la kiserikali-Population Service International limelenga kuwapatia watu aina mbili ya vidonge vya kusafisha maji kwa malipo madogo tu.Aina moja husaidia sana kupunguza hatari ya kupata tumbo la kuhara.Vidonge vya aina ya pili hupunguza hatari ya kujiambukiza kipindupindu na homa ya tumbo.Kwa njia hiyo gharama za kupata maji safi hupunguka na vile vile ni rahisi kusafirisha vidonge kuliko dawa ya klorini ambayo pia hutumiwa kusafisha maji hasa katika nchi zenye miundo mbinu iliyoendelea kwani klorini inafaa sana kuua bakteria zinazokutikana majini.