1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maji yazidi unga Misri

3 Julai 2013

Mvutano na wasiwasi umeongezeka Misri baada ya rais Mohammed Morsi kusisitiza hatong'atuka madarakani kama wanavyodai mamilioni ya waandamanaji wanaompinga.

https://p.dw.com/p/191Bj
Maandamano ya wapinzani uwanja wa al-Tahrir
Maandamano ya wapinzani uwanja wa al-TahrirPicha: Reuters

Wasiwasi watanda

Hali ya wasiwasi imetanda nchini Misri wakati wafuasi na wapinzani wa rais Mohammed Mursi wakiendelea na maandamano katika maeneo tofauti.Gazeti la serikali Al-Ahram limesema linamtarajia rais huyo mkaidi kuachia ngazi au kuondolewa kwa nguvu hii leo pale muda wa mwisho uliowekwa na jeshi utakapomalizika.

Maandamano ya wafuasi wa rais Morsi katika uwanja wa Raba El-Adwiya,Cairo.
Maandamano ya wafuasi wa rais Morsi katika uwanja wa Raba El-Adwiya,Cairo.Picha: Reuters

Hata hivyo duru za kijeshi zimekanusha taarifa zilizotangazwa na vyombo kadhaa vya habari nchini humo zinazotowa maelezo juu ya mpango wa amani wa jeshi utakaozingatiwa baada ya kumpindua madarakani rais huyo.Duru hizo za kijeshi zimesema taarifa hizo ni uvumi mtupu usiokuwa na chembe ya ukweli na kwamba kinachofikiwa na jeshi kwa hivi sasa endapo Mursi atakataa kusalimu amri ni kuitisha mkutano na vigogo wa kisiasa kijamii na kiuchumi nchini humo.

Chama cha Udugu wa kiislamu kimeshatoa cheche za maneno ya msimamo mkali ambapo naibu kiongozi wake Essam al-Erian ameonya kwamba watu wa taifa hilo hawatokaa kimya na kuangalia uasi wa jeshi.Tayari mapambano yameshuhudiwa usiku wa kuamkia leo kati ya wafuasi wa Mursi na wapinzani ambapo kiasi watu 23 wameuwawa wengi wao katika vurugu zilizotokea nje ya chuo kikuu cha mjini Cairo. Huku hatma ya kisiasa ikiwa katika wizani Rais Mursi analitaka jeshi kufutilia mbali muda wa mwisho iliyoutangaza wa saa 48 unaofikia kikomo jioni ya leo akisema hawezi kuridhia amri kutoka ndani au nje ya taifa hilo.

Mkuu wa jeshi Misri Abdel-Fattah al-Sissi
Mkuu wa jeshi Misri Abdel-Fattah al-SissiPicha: picture-alliance/dpa

Shinikizo zaidi dhidi ya Morsi

Mursi anazidi kukabiliwa na shinikizo hata kutoka kwa washirika wake serikalini,hivi punde kundi la Gamaa Islamiya zamani kundi la wanamgambo,ambalo limekuwa ni miongoni mwa washirika wachache waliobakia kumuunga mkono,limemtolea mwito kiongozi huyo kuitisha uchaguzi wa mapema ili kuepusha umwagikaji wa damu na mapinduzi ya kijeshi.Tarek al-Zumar afisa wa ngazi ya juu ndani ya kundi hilo amemwambia rais Mursi kuitisha uchaguzi wa mapema ni njia pekee ambayo pia itailinda katiba iliyopitishwa kuwa sheria mwezi Desemba.

Rais Mohammed Morsi
Rais Mohammed MorsiPicha: OZAN KOSE/AFP/Getty Images

Jumanne wasemaji watatu wa serikali wakiwemo wasemaji wawili wa rais huyo walijiuzulu.Hata hivyo hadi sasa kauli za Mursi na chama chake cha Udugu wa kiislamu kinaonesha kuwa tayari kupambana na jeshi huku pia kukionekana ishara za kuzuka mapambano kamili kati ya wapinzani na wafuasi wa Mursi.

Msimamo wa upinzani

Wapinzani wa Mursi wanasema rais huyo ameshapoteza uhalali wake kupitia makosa kadhaa pamoja na unyakuzi wa madaraka na kujitokeza kwa mamilioni ya watu katika uwanja wa Tahrir kunaonyesha wazi kwamba taifa zima haliko pamoja nae.Vyombo vya habari ndani ya Misri vinahesabu saa huku televisheni moja inayompinga rais huyo ikitangaza kwamba muda wake wa mwisho ni saa kumi jioni saa za Misri. Ripoti zinasema Benki kuu ya taifa hilo imetowa amri kwa mabenki yote kufunga milango yao kufikia saa nane mchana saa za Misri,kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na jeshi kumalizika.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/dpa/Rtre

Mhariri:Josephat Charo