1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majimbo ya mashariki mwa Ukraine yawachagua viongozi

3 Novemba 2014

Majimbo ya waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine yamewachagua viongozi wao katika uchaguzi ambao matokeo yake yametambuliwa na Urusi na kukataliwa na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/1DfwK
Ostukraine Wahlen Donezk 02.11.2014
Picha: Reuters/Maxim Zmeyev

Mambo yalikwenda kama yalivyotarajiwa hapo jana katika jimbo ambalo waasi wanaliita Jamhuri ya Watu wa Donetsk na jimbo jirani la Jamhuri ya Watu wa Luhansk, huku wagombea wote wawili walioongoza uchaguzi huo wakishinda kwa urahisi.

Matokeo ya mwanzo ya wapiga kura yalionesha kuwa Alexander Zakharcheko, mwenye umri wa miaka 38, ambaye ni kiongozi wa waasi wanapigana na wanajeshi wa Ukraine mjini Donestk alipata zaidi ya asilimia 80 ya kura. Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Zakharchenko alisema bado wako tayari kwa mazungumzo na serikali ya mjini Kiev . "Inasikitisha kuwa bado hatuelewi sera ambazo serikali ya mjini Kiev imetutengea. Kwa muda mrefu tumetaka kuzugnumza na serikali ya Ukraine. Tunasubiri jibu sahihi kutoka kwao.

Alexander Sachartschenko Donezk Wahlen Ostukraine 02.11.2014
Alexander Zakharchenko amechaguliwa kama waziri mkuu wa jimbo linalojiita Jamhuri ya Watu wa DonetskPicha: Alexander Khudoteply/AFP/Getty Images

Katika eneo la Luhansk, Igor Plotnitsky mwenye umri wa miaka 50, hakufanya vyema sana, lakini anaripotiwa kupta zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa. Na kama tu matokeo hayo yalivyotabiriwa, hivyo ndivyo kauli za Urusi na nchi za Magharibi zilivyokuwa. Urusi iliyaidhinisha maramoja matokeo ya uchaguzi huo.

Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ilisema Urusi inaheshimu nia ya wakaazi wa kusini mashariki mwa Ukraine ikiongeza kuwa waliochaguliwa wana jukumu la kuyatatua masuala ya kimsingi ya kurejesha utulivu na maisha ya kawaida katika eneo hilo. "Umoja wa Ulaya umepinga uchaguzi huo, huku mkuu wake mpya wa sera za kigeni Federica Mogherini akisema utavuruga hata zaidi juhudi za kuleta amani katika eneo hilo linalokabiliwa na machafuko. Taarifa kutoka kwa ofisi ya Mogherini imesema uchaguzi huo siyo halali na usiokubalika, na kuwa Umoja wa Ulaya hauwezi kuutambua".

Akizungumza leo wakati wa ziara nchini Indonesia, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema Ujerumani inaunga mkono kikamilifu matamshi ya Mogherini. " Ninasema wazi kuwa kile kilichoitwa uchaguzi, uliofanyika mashariki mwa Ukraine, haukuzingatia nia ya makubaliano ya Minsk, na hivyo tunakubaliana na kauli ya Umoja wa Ulaya kuwa uchaguzi huu hauwezi kukubalika".

Kura hizo pia zimekosolewa na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya – OSCE, ambalo Urusi ni mwanachama. Pia limesema uchaguzi huo ulikiuka makubaliano yaliyosainiwa mjini Minsk mwezi Septemba, ambayo, yalipunguza mapigano mashariki mwa Ukraine.

Mwandishi: Bruce Amani (Reuters, AFP, dpa, AP)
Mhariri:Josephat Charo