1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari mbioni kutaja Baraza lake la Mawaziri

Mjahida6 Oktoba 2015

Baraza la Senate la Nigeria limetangaza majina ya watu 20 walioteuliwa kuwepo katika baraza la mawaziri la rais Muhammadu Buhari, wanaowasilisha maeneo yote ya taifa hilo la Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/1GjZv
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Miongoni mwa wagombea waliotajwa ni pamoja na gavana wa zamani wa jimbo la Lagos, Babatunde Fashola, gavana wa zamani wa Rivers Rotimi Amaechi na mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu Kayode Fayemi. Hata hivyo Buhari hakusema wazi ni vyeo gani vitakavyoshikiliwa na watu hao.

Orodha ya Buhari imekuja zaidi ya miezi sita tangu alipochaguliwa hatua iliyoonekana kuwa ya mabadiliko ya kwanza ya kidemokrasia katika taifa hilo linalozalisha mafuta kwa wingi barani Afrika. Rais huyo wa Nigeria aliyekuwa dikteta wa kijeshi kwa muda mfupi miaka 30 iliyopita, amesema ana nia ya kuiondoa Nigeria ndani ya masuala ya rushwa.

Hata hivyo orodha iliyotolewa ya baraza la mawaziri inajumuisha pia wanachama wa chama cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan kilichoungana na Buhari na kumpa kiongozi huyo wa kiislamu wa eneo la Kaskazini kura za watu wa eneo la Kusini.

Shirika la kitaifa la mafuta Nigeria NNPC
Shirika la kitaifa la mafuta Nigeria NNPCPicha: Reuters/A. Sotunde

Rais wa Bunge la senate Bukola Saraki amesema rais Buhari pia amemuuliza mkuu wa shirikala la kitaifa la mafuta NNPC Emmanuel Ibe Kachikwu, kujiunga na baraza lake. Saraki aliyekuwa akisoma majina ya walioteuliwa na Buhari yanayohitaji kupitishwa katika baraza la wawakilishi, hakusema ni nafasi gani atakayoichukua Kachikwu.

Lakini duru zinasema anatarajiwa kuwa waziri wa mafuta katika jimbo lake atakayekuwa chini ya Buhari na atakayeangalia shughuli za kila siku katika sekta hiyo muhimu. Wiki iliyopita rais Buhari alisema yeye ndiye atakayeiongoza wizara hiyo.

Buhari aapa kupambana na rushwa ndani ya serikali yake

Wanawake walioteuliwa ni pamoja na mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa Amina Ibrahim na Kemi Adeosun, kamishna wa fedha wa zamani anayepambana na rushwa.

Orodha hiyo ilikabidhiwa baraza la senate tarehe 30 mwezi Septemba lakini majina bado hayajatolewa yote hadharani kwa kuwa maseneta wapo mapumzikoni. Hata hivyo majina zaidi ya walioteluliwa yanatarajiwa kutolewa katika siku zijazo.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

Rais Muhammadu Buhari amekuwa akiiendesha Nigeria kupitia wafanyakazi wa ummah katika wizara za serikali tangu alipoapishwa rasmi tarehe 29 mwezi May mwaka huu. Kabla ya kuchukua rasmi madaraka Buhari alisema rushwa pamoja na mafisadi hawatakuwa na nafasi katika serikali yake, huku hatua ya kuwachuja wagombea ikionekana kuwa sababu ya kuchelewa kuwateua viongozi wa wizara za nchi hiyo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/REUTERS

Mhariri: Josephat Charo