1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majonzi ya Wazimbabwe

P.Martin10 Agosti 2007

Hii leo ni miaka saba tangu wakulima wa kizungu kuanza kufukuzwa mashambani mwao nchini Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/CB22
Wateja wakisukumana dukani mjini Harare,baada ya bei za bidhaa kushushwa kwa amri
Wateja wakisukumana dukani mjini Harare,baada ya bei za bidhaa kushushwa kwa amriPicha: AP

Tangu ilipochukuliwa hatua hiyo katika mwaka 2000,serikali ya Rais Robert Mugabe takriban imetengwa na jumuiya ya kimataifa.Uchumi wa nchi hiyo pia umeporomoka.

Wengi hutokwa na machozi wanapoona kile kilichoifika Zimbabwe,miaka 27 baada ya uhuru wake.Wanachoona ni majonzi,vitisho na zaidi ya watu milioni 3 wanaotegemea msaada wa chakula kutoka nje.Vile vile mfumuko wa bei umepindukia asilimia 4,500 hadi serikali kuchukua hatua ya kudhibiti bei za bidhaa.

Kila siku,si chini ya watu 3,000 huondoka Zimbabwe,miongoni mwao wakiwemo madaktari,walimu na wakulima.Wanaondoka makwao,kwa sababu maisha yamefanywa kuwa magumu;na aliesababisha hali hiyo ni mmoja-Rais Robert Mugabe ambae ni rais wa kwanza na hadi hivi sasa ni rais pekee wa Zimbabwe akinga´ngania kwa nguvu madaraka hayo,hata ikiwa kwa kufanya hivyo,nchi yake inateketea.

Janga hilo lilianza miaka saba iliyopita. Alipohofia kuwepo uwezekano wa kunyanganywa kura nyingi za wapiga kura na chama cha upinzani cha MDC,kilichoundwa upya wakati huo,Mugabe alitangaza vita.Waafrika dhidi ya wazungu. Wakulima wadogo dhidi ya wakulima wakubwa.Takwimu zilihalalisha hatua zake,kwani asilimia 70 ya mashamba ya kibiashara yalikuwa katika mikono ya wazungu.Kwa hivyo maelfu ya wakulima walinyanganywa mashamba bila ya kulipwa fidia.

Hapo hapo wengi walitambua kuwa nchi haiwezi kujengwa kwa takwimu tu,hata ikiwa ni za kweli.Si hilo tu bali Mugabe alificha ukweli kwamba baadhi kubwa ya wakulima wa kizungu walinunua mashamba yao baada ya uhuru na kwa idhini ya serikali yake mwenyewe.

Hata uasi ulioandaliwa na kufanywa na Waafrika wasio na chochote haukotokea papo hapo.Wale waliosemekana kuwa wakongwe wa vita,walikuwa hata hawajazaliwa wakati wa vita vya kugombea uhuru. Watu hao walivamia mashamba ya wazungu,waliwabaka wake wa wakulima hao na kuwapiga vibaya wanaume.Wengine waliuawa na wengi walifukuzwa ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa Kiafrika wa mashamba hayo.Ghafula maelfu ya watu hao hawakuwa na kazi wala mahala pa kuishi.

Wakati uchumi wa nchi ulikuwa ukiteketezwa kwa machafuko,mahakama huru pia zilaanza kulengwa na Mugabe.Mahakimu wa kesi zilizohusika na mashamba yaliyonyangánywa,walipoamua kuwa hatua hiyo si halali walishinikizwa kwa vitisho hadi kujiuzulu wenyewe.Watu waliponyanyaswa,polisi walitazama tu,kama uonevu huo ulitendwa kwa jina la rais.

Hayo ni mambo yanayowasikitisha wengi na kwa haki,kwani hadi hivi sasa,hawakupata cho chote isipokuwa dhiki.Hata wakulima waliotaraji kufanikiwa kutokana na mageuzi yaliosemekana kuwa yatanufaisha maelfu ya watu,wamepoteza kila kitu.

Mara nyingine,Wazimbabwe hujiuliza,vipi mambo yameweza kufikia hali kama hiyo?Na ulimwengu uko wapi?Kwani vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kwa mfano,wala havikuzuia ukiukaji wa haki za binadamu.Havikuzuia pia watu kuikimbia nchi.

Kwa sababu hiyo,wengi wanatokwa na machozi wanapoifikiria Zimbabwe,Waafrika kwa Wazungu, kwani hatimae,wote ni wahanga wanaotaka mustakabali ulio bora.