1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaazi ya walowezi yaongezeka kwa asilimia 70.

Mohamed Abdulrahman18 Oktoba 2013

Ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la ukingo wa magharibi umeongezeka kwa asili mia 70 mwaka huu. Hayo ni kwa mujibu wa kundi la linalopinga ujenzi wa makaazi hayo linalojiita " Amani sasa."

https://p.dw.com/p/1A2Cj
Makaazi ya walowezi
Makaazi ya waloweziPicha: Reuters

Licha ya ripoti kwamba Israel imekuwa kimya kimya ikichelewesha ujenzi mpya wa makaazi hayo, hata hivyo inaelezwa kwamba takwimu hizo ni za kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu 2013, kabla ya kuanza tena amazungumzo ya amani kati ya Israel na Wapalestina mwezi Julai.

Wadadisi wanasema huenda hali hiyo ikizidisha wasiwasi wa wapalestina kuhusu kasi ya ujenzi wa makaazi katika ardhi yao inayokaliwa na ambayo wanataka iwe dola yao ya baadae.

Kwa mujibu wa kundi hilo la Amani sasa ambalo linapinga ujenzi wa makaazi katika maeneo yaliotekwa na Israel katika vita vya Mashariki ya Kati 1967, kulikuwa na nyumba 1,708 kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu ikilinganishwa na 995 wakati wa kipindi sawa na hicho mwaka jana 2012.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters

Asilimia 61 ya makaazi hayo yako katika maeneo yaliotengwa,nje ya ujenzi mkubwa wa makaazi ambayo Israel inasema inakusudia kuyabakisha hata katika makubaliano yoyote ya amani ya baadae na wapalestina.

Mei mwaka huu, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba waziri mkuu Benjamin Netanyahu ameamuru kuzuiwa kwa kandarasi mpya za ujenzi wa miradi mipya ya nyumba, katika kile kinachoangaliwa kuwa ni hatua ya kusaidia kuyafufua mazungumzo ya amani yanayoungwa mkono na Marekani na ambayo yalikwama kwa miaka mitatu.

Jumuiya ya Amani sasa yatoa tamko

Jumuiya ya "Amani sasa", inasema hakuna majaribio mapya ya maombi ya ujenzi yaliofanywa tangu ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani mwezi Machi.

Lakini katika ripoti yake mpya inasema kuzuiwa tenda hakuna athari yoyote kwa ujenzi kwa sababu 86 asili mia ya makaazi yalioanza miezi 6 iliopita yamejengwa katika maeneo ambako kibali hakihitajiki.

Mshirika muhimu katika serikali ya mseto ya Netanyahu-chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Jewish Home na wanachama wa Likud cha Netanyahu wamemtaka aendelee kuimarisha ujenzi wa makaazi.

Makaazi yaliojengwa na Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi na Mashariki ya Jerusalem yanazingatiwa na nchi nyingi duniani kuwa si halali lakini Israel inasema ni maeneo yake ya Kihistoria kulingana na Biblia, ambako sasa kunaishi waisraili wapatao 500,000 kandoni mwa wapalestina milioni 2 na nusu.

Rais wa Marekani Barrack Obama na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Rais wa Marekani Barrack Obama na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters

Katika ukurasa wake wa uhariri kwenye mtandao, Jumuiya ya Amani Sasa, imesema wakati makaazi yanaweza kuondoa hali ya kuaminiana baina ya Israel na Wapalestina, pia yameliuwa lile suluhisho la dola mbili.

Jumuiya hiyo inasema idadi ya makaazi katika Ukingo wa Magharibi imeongezeka mara tatu tangu uliposainiwa mkataba wa mpito wa Oslo miaka 20 iliopita,lakini asili mia 64 yako katika maeneo ambayo huenda Israel ikashikilia yabakie katika mamlaka yake wakati wa makubaliano yoyote ya amani na Wapalestina.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/ Reuters

Mhariri: Abdul Mtullya