1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makabiliano katika ikulu Tunisia

17 Januari 2011

Jeshi la Tunisia linakabiliana na walinzi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo. Pameripotiwa ufyatulianaji risasi karibu na ikulu mjini Carthage.

https://p.dw.com/p/zyUI
Serikali ya mpito Tunisia inatarajiwa kutangazwa leoPicha: AP

Kabla ya makabiliano hayo ya risasi hapo jana jioni, hali ya usalama nchini humo iliimarika na hali ya hatari iliyotangazwa siku ya Ijumaa, ilipunguzwa kuwa amri ya kutotembea usiku. Serikali ya mpito inatarajiwa kutangazwa hii leo na itajumuisha wanachama wa vyama vitatu vya upinzani badala ya wanachama wa chama tawala kilichokuwepo.Hapo awali rais wa mpito aliapishwa na alimuomba waziri mkuu, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, ikijumuisha pia wajumbe kutoka vyama vya upinzani.

Übergangspräsident Mebazaa Tunesien
Rais wa mpito Fouad MebazaaPicha: AP

Kuapishwa Rais Mebazaa

Rais wa muda wa nchi hiyo, Fouad Mebazaa, aliapishwa baada ya Ben Ali na familia yake kukimbilia nchini Saudi Arabia. Hapo jana Waziri Mkuu Mohammed Ghannouchi alikuwa na majadiliano na vyama vyote vya kisiasa kuhusu uundaji wa serikali. Wakati huo huo, taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zinasema kuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Rafik Belhajj, pamoja na Mkuu wa Kikosi Maalum cha Rais wanashikiliwa na polisi na huenda wakafikishwa mahakamani kwa kuchochea machafuko ambayo hadi sasa yamechukuwa maisha ya watu 90.

Ben Ali mkimbizi wa kisiasa

Zine El Abidine Ben Ali
Picha: picture alliance / dpa

Kwa upande mwengine, Saudi Arabia imenyamaa kimya juu ya shughuli za Rais wa Tunisia aliyeikimbia nchi yake, Zine al-Abidine Ben Ali, na kwenda Jeddah. Inasekana Saudi Arabia inampokea Ben Ali kama mkimbizi wa kisiasa na sio kama mkuu wa nchi, hataruhusiwa kutoa taarifa za kisiasa au kuendesha shughuli za kisiasa, na kwa mujibu wa mchambuzi mmoja hataruhusiwa kuwasiliana na mtu yeyote huko Tunisia.

Mwandishi: Maryam Abdalla, Khelef Mohammed /Dpa/Rtre