1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makabiliano ya risasi yaendelea Cote d'Ivoire

John Juma
7 Januari 2017

Mapigano ya risasi yametokea katika miji kadhaa nchini Cote d'Ivoire, likiwemo jiji kuu na la kibishara Abidjan. Kulingana na wanajeshi na raia, mapigano hayo yalianza usiku wa kuamkia leo na kuendelea hadi asubuhi

https://p.dw.com/p/2VRcy
Elfenbeinküste Bouake Unruhen
Picha: Reuters

Mapigano ya risasi yametokea katika miji kadhaa nchini Cote d'Ivoire, likiwemo jiji kuu na la kibishara Abidjan. Kulingana na wanajeshi na raia, mapigano hayo yalianza usiku wa kuamkia leo na kuendelea hadi asubuhi. Hiyo ikiwa dalili ya kushamiri kwa mamalamiko ya wanajeshi waasi wanaotaka nyongeza ya mishahara na marupurupu.

Wanajeshi walidhibiti jiji la pili kwa ukubwa Bouake mapema leo. Waasi nao wakatapakaa hadi katika miji mingine minne mikuu, huku serikali ikijaribu kutuliza ghasia kwa kuahidi mazungumzo na waasi hao wanaoendeleza uhaini.

Makabiliano makali yalisikika usiku katika mji ulioko kaskazini mwa mji wa Korhogo na mapema leo yakatokea katika mji wa Bouake. Baadaye, raia na wanajeshi waliripoti kutokea kwa ufyatulianaji risasi katika mji wa Man Toulepleu na katika kambi kuu ya jeshi iliyoko jijini Abidjan. Jiji lenye jumla ya wakaazi milioni 5, kando na kuwa ndiko ziliko ofisi ya rais, za serikali na bunge.

‘‘Ufyatuaji risasi umeanza sasa katika kambi yetu pia.'' Amesema mwanajeshi mmoja katika kambi ya Akouedo iliyoko katika sehemu wanakoishi watu jijini Abidjan. Mapigano hayo pia yamethibitishwa na mkaazi mmoja wa eneo hilo.

Nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inayotumia Kifaransa, imeinuka kutoka katika mzozo wa kisiasa wa kati ya mwaka 2002 hadi 2011 na kuwa mojawapo ya nchi zinazoinukia kiuchumi barani Afrika.

Hata hivyo kufuatia miaka mingi ya migogoro na kushindwa kufanyia mageuzi jeshi lake ambalo linajumuisha waasi wa zamani na wa serikali, kumeifanya nchi hiyo kukumbwa na migawanyiko ya ndani kwa ndani.

Mapema leo, wanajeshi waasi walidhibiti maeneo muhimu ya kuingia katika mji wa Bouake, na kusababisha makabiliano kati ya waasi hao na vikosi vilivyotumwa kutoka Abidjan kuimarisha usalama. Ufyatulianaji wa risasi ulianza saa kumi na mbili alfajiri, katika mji wa Bouake ulio na takriban wakaazi nusu milioni.

Wanajeshi katika kizuizi cha barabara mjini Bouake
Wanajeshi katika kizuizi cha barabara mjini BouakePicha: Reuters

Haikufahamika moja kwa moja nini kilisababisha mapigano hayo, lakini mmoja wa wanajeshi waasi alisema, waliona mienendo ya kutilia shaka nje ya kambi ya kijeshi ya Bouake. ‘‘Haya ni makabiliano kwa kutumia guruneti ili kuwazuia'' Alisema

Mwandishi mmoja wa shirika la habari la Reuters aliyeingia Bouake siku ya Ijumaa na kuzungumza na baadhi ya waasi hao, amesema, wengi wao ni wanajeshi wa ngazi za chini pamoja na wapiganaji waliovunjika mioyo.

Karibu wote walionekana kuwa wanachama wa kundi jipya la uasi ambalo limetumia Bouake kama makao yake makuu, na kudhibiti nusu ya kaskazini ya Cote d'Ivoire tangu 2002 hadi nchi ilipounganishwa mwaka 2011 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Katika taarifa yake mnamo Ijumaa jioni, waziri wa ulinzi Alain-Richard Donwahi alitoa wito wa utulivu na kuwa serikali ipo tayari kusikiliza malalamiko yao, hasa baada ya uasi huo kujipenyeza hadi miji ya Daloa, Daoukro na Odienne.

Akisema kuwa wito wa uasi huo unaeleweka, lakini ni mbaya, kando na kuwa inatoa picha mbaya ya nchi. Amesema ataelekea Bouake kuzungumza na wanajeshi hao waasi.

Bema Fofana ambaye ni mbunge anayewakilisha Bouake, amesema wanajeshi hao walikubali Ijumaa kuwa wangerejea kambini Jumamosi asubuhi. Lakini saa kadhaa baadaye, hali katika barabara haikuwa imerejea kama kawaida, amesema mwanahabari mmoja anayetokea eneo hilo. Ameongeza kuwa ‘‘Wameshikilia pale pale maeneo walikokuwepo. Wangali katika maeneo ya kuingia katika jiji na mizunguko iliyoko katikati ya jiji. Mwanahabari huyo hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama.

Mwandishi: John Juma/RTRE
Mhariri: Bruce Amani