1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi ya pamoja yagunduliwa Burundi

Admin.WagnerD29 Januari 2016

Shirika linalopigania haki za binaadamu la Amnesty International limesema picha zilizopatikana kwa kupitia satelaiti, zikionaonesha idadi kubwa ya watu waliouawa na vikosi vya usalama vya Burundi mwezi Desemba mwaka jana

https://p.dw.com/p/1Hlgw
Burundi Polizeigewalt - Polizei schlägt Jungen
Polisi wakimpiga kijana mwandamanaji mjini BujumburaPicha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Shirika hilo la haki za binaadamu linasema kuna uwezekano wa kuwepo makaburi yasiyopungua matano katika eneo la Buringa- kwenye vitongoji vya jiji la Bujumbura. Picha zilizopigwa mwishoni mwa mwezi wa Desemba na mapema Januari zinaonyesha ardhi iliyochimbwachimbwa. Shuhuda mmoja aliliambia shirika la Amnesty Internationa kwamba makaburi hayo yalichimbwa jioni ya Desemba 11, muda mfupi baada ya siku ya maafa ya mauwaji makubwa mjini Bujumbura.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Amnsety, mashuhuda walielezea kwa jinsi gani polisi na maafisa wengine wa serikali katika eneo la Nyakabinga na mengine ya jirani walivyokusanya miili ya waliouwawa na kuipelekea katika eneo lisilojulikana.

Makaburi ya pamoja

Duru zinaeleza watu 25 walizikwa katika makaburi matano katika eneo la Mpanda, na miili mingine 28 ilizikwa katika eneo la makaburi ya Kanyosha nchini humo.

Mapema mwezi huu, mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Zeid Raad al-Hussein vilevile alitoa wito uchunguzi wa haraka kufuatia tuhuma ya uwepo wa makaburi ya pamoja. Zeid alitaja kile alichokiita "kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa haki za binaadamu,"kwa kusema madai yameongezeka juu ya watu wanaotoweshwa, kuwepo kwa vizuizi vya siri na makaburi ya pamoja.

Serikali ya Burundi imekanusha tuhuma zote, kwa kusema umoja huo wa mataifa umejiegemeza katika taarifa potofu zenye kusambazwa na wapinzani wa utawala huo ambao wanaishi uhamishoni. Msemaji wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba alisema Umoja wa Mataifa upo huru kwenda Burundi na kuchunguza tuhuma zote, ambazo alisema zina lengo la kuijengea taswira Burundi, kama taifa hatari sana.

Katika mashambulizi ya kupangwa, watu wenye silaha walishambulia maeneo matatu ya kijeshi Desemba 11. Na siku iliyofuata, watu 28 walikutwa wameuwawa katika maeneo ya jiji la Bujumbura. Mashuhuda waliliambia shirika la habari la AP miongoni mwao waliokufa ni kutokana na mashambulizi hayo.

Shuhuda mwingine alilalamika kuwa vikosi vya usalama vilikuwa wakiwasaka watu nyumba hadi nyumba.

Uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza, kuwania muhula mwingine wa tatu wa Aprili mwaka jana, ulisababisha watu kuingia barabarani, na kusababisha vilevile jaribio la mapinduzi lililofeli mwezi Mei na uasi ulisababisha taifa hilo kuelekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wapinzani na wafuasi wa Nkurunziza wamekuwa wakiwindana wenyewe kwa wenyewe kwa bunduki,maroketi na silaha nyingine wakati vurugu zikizagaa hadi katika majimbo mengine ya Burundi.

Mwandishi: Sudi Mnette/APE
Mhariri:Daniel Gakuba