1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makadirio ya kiuchumi nchini Ujerumani

Oumilkher Hamidou23 Aprili 2009

Taasisi mashuhuri zaashiria hali mbaya ya kiuchumi hadi mwaka 2010

https://p.dw.com/p/HcjF
Kai Carstensen(wa kwanza kushoto) wa taasisi ya IFO ya mjini MunichPicha: AP

Taasisi mashuhuri za kiuchumi kutoka Ujerumani,Austria na Uswisi zinaashiria shughuli za kiuchumi nchini Ujerumani zitaporomoka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hadi sasa.Uchumi utaporomoka kwa asili mia 6 mwaka huu.kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu shirikisho la jamhuri ya Ujerumani lilipoundwa.Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya msimu wa kiangazi iliyotangazwa na taasisi hizo hii leo mjini Berlin.

Hata wataalam wanaweza kukosea.Msimu wa mapukutiko uliopita,taasisi zinazoongoza za kiuchumi ziliashiria ukuaji wa kiuchumi wa asili mia sifuri nukta mbili kwa mwaka huu wa 2009.Katika ripoti ya msimu huu wa kiangazi lakini hali ya mambo ni nyengine kabisa,kama anavyosema Kai Carstensen wa taasisi ya IFO ya mjini Munich:

"Katika msimu huu wa kiangazi wa mwaka 2009,uchumi wa Ujerumani unajikutqa katika hali ya kuzorota,hali ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu shirikisho la jamhuri ya Ujerumani lilipoundwa.Pato la ndani litapungua kwa asili mia 6 kwa mwaka huu wa 2009.Taasisi hazitarajii mabadiliko ya maana kwa mwaka wa 2010.Pato la ndani linaweza kuteremka kwa asili mia sifuri nukta tano."

Lakini Kai Carstensen anasema pia kwamba nakisi ya asili mia sita katika pato la ndani inasabishwa na kupungua shughuli za viwandani kwa msimu wa baridi uliopita.Bwana Kai Carstensen anaamini zilzala hasa imeshapita,kinachoshuhudiwa hivi sasa ni dharuba ndogo ndogo na safisha safisha na hasa katika soko la ajira.Dharuba hizo ndogo ndogo na madhara yake katika soko la ajira, anaamini mtaalm huyo wa taasisi ya kiuchumi ya mjini Munich,zitachukua muda hadi kumalizika na zitaleta madhara pia.

Makampuni mengi yanaweza kuvuta pumzi kidogo,lakini kwa muda wote ule ambao shughuli za kiuchumi hazitaanza kunawiri,mashirika hayo hayataweza kuwaajiri watu wengi.Nafasi milioni moja za kazi zitafutwa,katika kipindi cha miezi ijayo,wanaashiria wataalm hao.Hadi mwishoni mwa mwaka 2010,idadi ya wasiokua na kazi inaweza kuongezeka na kufikia watu milioni tano.Ni picha ya kutisha hiyo inayojitokeza ikifuatiwa na nakisi inayozidi kuongezeka ya bajeti.Kwa mwaka huu wa 2009,nakisi hiyo inatazamiwa kufikia yuro bilioni 89.Kiwango hicho kinafikia asili mia 3,5.Na kutokana na uwezekano wa kuzidi idadi ya wasiokua na kazi na kupungua shughuli za kiuchumi kiwango cha nakisi ya bajeti kinatazamiwa kufikia asili mia 5.5,kwa maneno mengine yuro bilioni 133 kwa mwaka ujao wa 2010.

Muda gani utahitajika hadi hali ya mambo itakapoanza kuimarika nchini Ujerumani,wataalam wanakubaliana itategemea hali jumla ya kiuchumi ulimwenguni.


Mwandishi:Sabine Kinkartz/ZR / O.Hamidou

Mhariri:M.Abdul-Rahman