1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makala maalum: Umuhimu wa mtandao wa Internet

Katrin Ogunsade / Maja Dreyer25 Juni 2007

Kwa Waafrika wanaoishi mbali na nyumbani kwao, mtandao wa Internet ni chombo muhimu sana ambacho wengi wanakitumia kila siku wakiwasiliana na wenzao wa nyumbani, lakini pia kupata marafiki katika nchi ya kigeni waliko.

https://p.dw.com/p/CHkR

Kuna karasa fulani kwenye mtandao huu ambazo zinatumika kama jukwaa la kubadilishana habari na kushauriana, mfano mmoja ni ukarasa wa “youngafrican.com”. Hapa Ujerumani, Watanzania wanatumia ukarasa mwingine uitwao “kilimandjaro.com” kwa ajili ya kuwasiliana. Basi jukwaa hilo lina maana gani katika maisha ya vijana kutoka Tanzania walioko Ujerumani. Mwenzetu Katrin Ogunsade alikutana nao mjini Cologne:

Kuna sufuria kubwa ya Pilau mezani na muziki wa Kiswahili unasikika – ni kama nyumbani pale Harold Ishehabi anapokutana na wenzake wa Tanzania. Kwa mara nyingine tena, Harold ambaye anafanya kazi kwenye chuo kikuu cha Aachen, amekuja Cologne kuwaona marafiki zake. Zamani, mikutano kama hiyo haikufanyika mara nyingi, kwani miaka ya kwanza nchini Ujerumani ilikuwa migumu, Harold anakumbuka. Hakujua kwamba kuna Watanzania wengi nchini humu.

Harold Ishebahi anatoka Bukoba, Tanzania, na amekuja Ujerumani kusoma. Maisha ya Ujerumani, tamaduni za hapa, lugha yenyewe – hakuna mtu aliyemsaidia. Hatimaye alikutana na bibi moja wa kutoka Tanzania. Kwa pamoja walikuwa na wazo: “Tukadhani ikiwa tungekuwa na jukwaa la kuzungumzia, tutakuwa na fursa ya kuunda mtandao wa Watanzania walio sehemu tofauti za Ujerumani na kuwasiliana nao.”

Wakaanzisha basi ukarasa wa “kilimandjaro.de” ikiwa ni mahala pa kubadilishana barua pepe kati ya Watanzania walioko Ujerumani. Tangu wakati huo miaka sita iliyopita hadi leo kuna Watanzania mia moja hivi wanaotumia ukarasa huo. Mmoja kati ya watumiaji ni Grace Soko ambaye pia alikuja kwenye mkutano wa Cologne: “Natumia tovuti kwa madhumuni mbali mbali: Kupata habari na kubadilishana habari, juu ya nchi yangu na juu ya maisha ya hapa Ujerumani. Lakini pia kusaidiana.”

Miaka miwili iliyopita, marafiki zake wa “kilimandjaro.de” walimsaidia sana Grace. Wakati huo, mama yake alifariki dunia Tanzania. Ikambidi Grace kwenda nyumbani na kutumia pesa nyingi pale. Hata kulipa tiketi ya kurudi Ujerumani na kuendelea na masomo akakosa. Lakini, marafiki zake Watanzania wa Ujerumani walipata habari hizo na wakachangia kumlipia tiketi ya ndege. Hivyo, jukwaa hilo la pamoja kwenye tovuti ni muhimu sana katika maisha yake.

Kwa Harold na Watanzania wengine waliokutana Cologne ni hivyo hivyo. Harold anasema: “Kile tunachokifanya si kitu kipya, hata Tanzania si kitu kipya. Tuna ushirikiano mzuri katika jamii yetu. Lakini hapa Ujerumani tunaishi mahala tofauti yaliyo mbali. Kupitia tovuti sasa tuna uwezo wa kuja pamoja na kuwasiliana.”

Kwa pamoja wanatafuta suluhisho kwa matatizo ya chuo au kujadiliana juu ya masuala ya kisiasa. Mpango wao sasa ni kuongeza idadi ya watumiaji wa jukwaa lao.