1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makanisa yajitahidi kuimarisha amani Sudan Kusini

Jutta Schwengsbier / Maja Dreyer26 Julai 2007

Kwa mara nyingine tunaripoti juu ya mzozo katika eneo la Darfur, huko Magharibi mwa Sudan. Kinachosahauliwa ni juhudi za kuimarisha amani Kusini mwa nchi hiyo. Sasa ni miaka miwili tangu mkataba wa amani kati ya eneo hilo na serikali ya Khartoum kutiwa saini. Mwandishi wetu Jutta Schwengsbier ametembelea Sudan Kusini kuona vipi makanisa hasa yanajitolea katika kutafuta maridhiano.

https://p.dw.com/p/CHk0
Kuanza upya baada ya vita Kusini mwa Sudan
Kuanza upya baada ya vita Kusini mwa SudanPicha: AP

Milima ya Nuba iko katikati mwa Sudan kama mpaka kati ya eneo la Kusini na Kaskazini. Hapa ndipo palifanyika mapigano mengi ambayo baada ya mkataba wa amani kukubalika yamekwisha. Hata hivyo, kazi ya kuimarisha amani hii ni ngumu na itaendelea kwa muda, anasema askofu Andulu Adam Elnail ambaye ameanzisha jumuiya ya madhehebu mbalimbali ya kutafuta maelewano mjini Kadugli.

Askufu anaelezea zaidi: “Sisi tuna Waislamu na Wakristo katika familia moja. Watoto wa baba mmoja wanaweza kuwa Waislamu na wengine Wakristo. Wengine labda hawaamini kabisa. Lazima tuwalete pamoja watu wa hapa, la sivyo watauana yakitokea matatizo. Katika jumuiya yetu tunawafundisha vipi wanaweza kuisha pamoja kwa amani kwani Mungu amewaumba wote kuwa viumbe vya pekee.”

Wakati mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na amani yanazungumza hasa na makundi ya wanamgambo, makanisa yanajaribu kupatanisha. Maaskofu wanaonya kuwa wengi bado wanabeba silaha walizopewa na adui ili wawaue wenzao wa kabila jingine. Hata hivyo, mafanikio mengine yamepatikana kwa sababu makanisa yanaheshimika. Askofu mwingine Nataniel Garang anatupa mfano: “Wanawake wengi walitekwa nyara. Sasa makabila yanawarudisha nyumbani. Hii lakini ilikuwa kazi ngumu sana.”

Utaratibu ambao makanisa ya Sudan Kusini yanautumia kuleta maridhiano unazivutia pia nchi nyingine jirani ambazo zinakabiliana na hali ngumu ya kijamii baada mizozo na vita. Peter Tibi ambaye ni katibu mkuu wa Halmashauri ya makanisa ya Sudan Kusini ameshatembelea Ruana, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ethiopia na Eritrea kuzungumzia utaratibu huu.

Anaeleza kuwa ni mchangayiko wa mikakati ya kisasa na ya zamani kutatua mizozo. Hasa ni juu ya watu kukaribiana, anasema Peter Tibi: “Si juu ya kutoa na kuchukua, wala si suala la nani anashinda na nani ameshindwa. Lazia kwanza muhanga awe tayari kusamehe na yule aliyefanya maovu awe tayari kukubali makosa yake. Hapo maridhiano yanapatikana. Kitamaduni nchini Sudan lazima fidia ya damu ilipww. Tunaheshima desturi hiyo kwa hivyo baada ya mtu kukubali makosa yake hadharani tunachinja mbuzi au kondoo. Halafu tunakusanyika pamoja na kusali.”

Peter Tibi anakumbusha kuwa kulingana na desturi za Kiafrika, suala la kutatua mzozo si suala la kumwadhibu mhalifu, bali zaidi ni juu ya kurekebisha mahusiano kati ya binadamu. Ikawa mtu amawaua watu 20 au jamaa zangu wote, haitasaidia kama huyu pia anauawa. Iwapo mtu ameomba msamaha, hakuna haja tena kulipiza kisasi. Ili vita vimalizike lazima watu wazungumie chanzo cha mzozo na kufikia maafikiano.

Mara nyingine inabidi kutumia shinikizo la kijamii, kama anavyoeleza Peter Tibi: “Yule anayetaka kuendelea kupigana, yuko nje ya jumuiya. Yule ambaye haombi msahama, anafukuzwa kutoka jamii yake. Basi, kila mmoja anaweza kuamua mwenyewe ikiwa anataka kuwa peke yake au aingizwe katika kundi fulani ya jamii.”

Vita vimaharibu mshikamano katika jamii, anasema Peter Tibi. Kwa hivyo inabidi kaka na dada, watoto na wazazi waje pamoja tena ili amani iwe imara.