1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makocha wa kiafrika wanuwia kuwapiku wa kigeni

Admin.WagnerD5 Juni 2014

Makocha wa Kiafrika, Mghana Kwesi Appiah na Mnigeria Stephen Keshi wana shauku ya kufika duru ya pili katika Kombe la Dunia, na kuhitimisha miongo kadhaa ya kushindwa kwa makocha wa Kiafrika.

https://p.dw.com/p/1CCIk
Südafrika WM Fußball 2010
Picha: Getty Images

Tangu mwaka 1978, pale Mtunisia Abdelmajid Chetali alipokuwa kocha wa kwanza wa kiafrika kuiongoza nchi yake katika mashindano ya kombe la dunia, makocha wote 11 wa kiafrika waliofuatia wameshindwa kufuzu hatua ya mtoano. Licha ya rekodi hii mbaya, Appiah na Keshi ni waungaji wakubwa wa makocha wa Kiafrika, ingawa makocha watatu wa Ulaya wamelipatia matokeo bora zaidi, bara la Afika ambalo halijawahi kuvuka hatua ya robo fainali.

Mrusi Valery Nepomniachi aliiongoza Cameroon kufika nane bora mwaka 1990 na Mfaransa Bruno Metsu na Mserbia Milovan Rajevac walizifikisha katika hatua sawa Senegal mwaka 2002 na Ghana mwaka 2010. Katika mahojiano na chombo kimoja cha habari, kocha wa Nigeria Keshi alisema kuwa makocha weupe wanakuja Afrika tu kwa ajili ya kupata pesa na hawafanyi chochote ambacho wao makocha wa kiafrika hawezi kufanya.

Kocha wa Nigeria Stephen Keshi.
Kocha wa Nigeria Stephen Keshi.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

"Waafrika wanapoteuliwa kuzifundisha timu, wanatakiwa kushinda kila mechi ya kirafiki, kombe la mataifa ya Afrika na kombe la dunia," anasema Keshi na kuongeza kuwa inapokuja kwa wazungu, wao wanapewa mwaka mmoja kuzowea mazingira, kuijua vizuri nchi na wachezaji, jambo ambalo anasema siyo la ueledi.

Ubingwa unahitaji nguvu

Appiah kwa upande wake anatizama mbali ya raundi ya pili, na aliwaambia wandishi wa habari kuwa kikosi chake cha "Black Stars" kina nguvu ya kutosha kuweza kubeba kombe la dunia. Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana mwenye umri wa miaka 53, alisema kinchohitajika kuwa bingwa wa dunia ni kuwa na nguvu za kutosha.

Hata hivyo, kundi lake la raundi ya kwanza la G ambalo linazijumlisha pia timu kubwa za bara la Ulaya, Ujerumani na Ureno linatoa changamoto kubwa sana, hata kwa kikochi chenye vipaji cha Ghana. Keshi, ambaye aliichezea Nigeria wakati ikishiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza miaka 20 iliyopita, anaonekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuandika historia.

Wakati Argentina inapewa nafasi kubwa katika kundi F, Nigeria wanaweza kushika nao nafasi mbele ya Bosnia na Iran. Lakini Keshi mwenye umri wa miaka 52, hakubaliani na Wanigeria wanaodhani kuwa kufaulu litakuwa jambo jepesi kwa timu yao, na kusema litakuwa kosa kubwa sana kuzidharau Bosnia na Iran kwa kuwa nazo zilifaulu kufika hapo kama ilivyokuwa kwa Nigeria.

Mkakati wa mafanikio

Ili Ghana na Nigeria zifuzu kwenda mbele, Appiah na Keshi laazima wafaulu pale makocha nguli kama vile Mualgeria Rabah Saadane na Mmisri Mahmoud El-Gohary waliposhindwa. Makocha wawili wa Afrika Kaskazini - Mualgeria Rachid Mekhloufi na Mmorocco Mahieddine Khalaf, ndiyo walikaribia kuvuka raundi ya kwanza.

Walipanga vipigo vya kustukiza mwaka 1982 dhidi ya Ujerumani Magharibi nchini Uhispania na pia ushindi dhidi ya Chile. Lakini Algeria ilimalizia katika nafasi ya tatu kwa tofauti ya magoli baada ya waliofuzu, Ujerumani na Austria kucheza mechi ya mwisho ya kundi iliyotia aibu. Ushindi mwemamba wa Ujerumani ungehakikisha kuwa wao na Austria wanasonga mbele, na baada ya Ujerumani kuongoza dakika za mapema, mechi hiyo iligeuka kichekesho.

Kocha wa Ghana Kwesi Appiah.
Kocha wa Ghana Kwesi Appiah.Picha: Francisco Leong/AFP/Getty Images

Kwa bahati mbaya rekodi ya makocha wa Kiafrika tangu Algeria ilipoondolewa ni ya kufedhehesha, wakiwa na ushindi mmoja tu katika mechi 25 za kombe la dunia. Ushindi huo aliupata Jomo Sono, Nyota wa Afrika Kusini alienyimwa fursa na utawala wa ubaguzi wa rangi kuonyesha kipaji chake.

Mwanamfalme huyo mweusi kama alivyojulikana, aliifundisha nchi yake wakati wa mashindamo ya kombe la dunia mwaka 2002 nchini Korea Kusini na Japan, ambapo kikosi chake cha Bafanabafana kilifanikiwa kuishinda Slovenia. Lakini Uhispania na Paraguay zilifaulu, na kumuacha Sono katika nafasi ya tatu, kama ilivyokuwa kwa Mekhloufi na Khalef, Chetali na Muangola Luis Oliveira Gonclaves.

Timu zilizofundishwa mara mbili na Saadane, Watunisia Ali Selmi na Ammar Souayah, El-Gohary, Mmoroco Abdellah Blinda na Mnigeria Festus Onigbinde zote zilimaliza bila ushindi na zikiwa katika nafasi za mwisho. Sasa ni wakati wa Appiah na Keshi, na yatakuwa masikitiko makubwa sana ikiwa hakutakuwa na hata mmoja kati yao atakayevuka kizingiti hicho.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohamed Abudl-Rahman