1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makoni atangaza kuwania urais

Liongo, Aboubakary Jumaa5 Februari 2008

Waziri wa zamani wa fedha wa Zimbabwe, Simba Makoni ametangaza kuwania urais kama mgombea huru katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujayo nchini humo.

https://p.dw.com/p/D2vF
Rais Robert MugabePicha: AP

Wakati Simba Makoni akitangaza azma yake hiyo,upinzani kwa upande mwengine umeshindwa kuondoa tofauti zao na kuunganisha nguvu dhidi ya Rais Robert Mugabe katika uchaguzi huo.


Akitangaza uamuzi wake huo, Waziri huyo wa zamani wa Zimbabwe, amesema kuwa amefikia hatua hiyo baada ya kujadiliana kwa kina na baadhi ya wanachama wa chama cha ZANU PF.


Mbali na hao pia amesema kuwa amejadiliana na wanaharakati wengine waliyo nje ya chama hicho tawala cha ZANU PF kote nchini.


Simba Makoni mwenye umri wa miaka 57 amesisitiza kuwa anasimama akiwa mgombea huru na kwamba hana chama chochote.


Amesema kuwa alipenda kuwania urais kwa tiketi ya chama chake cha ZANU PF lakini hawezi kufanya hivyo, na kuongeza kwamba anajumuika na wananchi wa nchi hiyo wanaokabiliwa na madhila makubwa ya ugumu wa maisha kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.


Uchaguzi mkuu nchini humo umepangwa kufanyika tarehe 29 mwezi ujayo, ambapo Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 83 anawania kipindi cha sita cha uongozi.


Uamuzi wa Simba Makoni mtu anayeheshimika nchini Zimbabwe ameutoa baada ya mazungumzo ya vyama vya upinzani kuvunjika.


Chama cha MDC ambacho kimegawika pande mbili, kilikuwa katika mazungumzo ya kupanga mikakati ya kuunganisha nguvu kwa ajili ya uchaguzi huo.


Lakini kushindwa kwao na kutangaza kuwa kila chama kitasimamisha mgombea wake, kumewafanya wadadisi kuona kuwa kitendo hicho kinampa nafasi zaidi Rais Mugabe kushinda.


Bill Said ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Zimbabwe amesema kwa hatua hiyo upinzani hauwezi kukishinda chama cha ZANU PF pamoja na kwamba uongozi wa chama hicho umepelekea hali mbaya ya uchumi nchini humo.


Chama cha MDC kiligawika hapo mwaka 2005 kutokana na mzozo juu ya ushiriki katika uchaguzi wa bunge la seneta, lakini baada ya viongozi wa pande hizo mbili, Morgan Tsvangirai wa chama kikuu cha MDC na hasimu wake aliyejitenga Arthur Mutambara kupigwa na polisi mwezi March mwaka jana waliona haja ya kushirikiana.


Pamoja na kushindwa kukubaliana, kwa vyama hivyo, Morgan Tsvangirai amedai kuwa bado kuna nafasi ya kuweza kumshinda Mugabe.


Lakini Arthur Mutambara alikiri kuwa nafasi ya MDC kushinda uchaguzi huo ni finyu baada ya kushindwa kufikia muafaka.


Hata hivyo tangazo la Simba Makoni waziri wa zamani wa fedha wa Zimbabwe kuwania Urais akiwa mgombea huru, linaonekana kuwapa faraja wapinzani wa Mugabe.


Takavafira Zhou kutoka chuo kikuu cha Mavingo amesema kuwa kwa mara ya kwanza Mugabe atakabaliwa na upinzani mkali kutoka kwa mtu aliyekuwa naye karibu sana.


Chama cha MDC hakijasema lolote juu ya hatua ya Simba Makoni kutangaza azma yake hiyo, lakini upande wa kundi lililojitenga na MDC limeukaribisha uamuzi huo wa Makoni.


Msemaji wa kundi hilo Gabriel Chaibva alisema kuwa chama chake kinamkaribisha mtu yoyote ambaye yuko tayari kupambana na njaa, umasiki pamoja na udikteta wa Mugabe.