1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makosa makubwa yagunduliwa ushahidi wa FBI

Mohammed Khelef21 Aprili 2015

Marekani inaanza uchunguzi juu ya itifaki na taratibu za kimaabara zinazotumiwa na idara ya upepelezi (FBI) kufuatia ugunduzi wa karibuni kwamba ushahidi uliokusanywa kutoka maabara hizo ulikosewa.

https://p.dw.com/p/1FBa6
FBI-Logo
Nembo ya idara ya upelelezi ya Marekani (FBI).Picha: picture-alliance/dpa

Wizara ya Sheria imesema hivi leo kwamba uchunguzi huo utaangalia kwa nini makosa hayo ya kisayansi yalitokea na kuruhusiwa kuendelea kwa muda mrefu, huku vyombo vya usalama vikisema vitazipitia tena upya kesi zaidi ya mia moja, ambazo zinawezekana ushahidi wake uliotokana uchambuzi wa kisayansi wa nywele ulikuwa na makosa.

Hatua hizo zilizotolewa kwenye tamko hilo la pamoja kati ya taasisi ya Innocence Project na Chama cha Mawakili wa Utetezi wa Makosa ya Uhalifu nchini Marekani hivi leo zinafuatia ugunduzi ulioonesha kuwa ushahidi wenye makosa uliotolewa na wachunguzi maalum wa FBI umekuwepo kwa miongo mingi sasa. Makosa kwenye uchambuzi wa ushahidi wa nywele yamegunduliwa kwa visa vingi ambavyo vimepitiwa upya hadi sasa, wanasema maafisa wa serikali.

Wizara ya Sheria na FBI wamekubaliana kuzipitia upya kesi zote za uhalifu ambapo uchambuzi wa nywele ulisaidia kumuhusisha mshtakiwa na uhalifu alioshitakiwa nao, kufuatia kuachiwa huru kwa watu watatu ambao awali ushahidi kama huo ulitumika dhidi yao. Uchunguzi huu wa sasa unarudi hadi kwenye kesi zilizohukumiwa kabla ya mwaka 2000, wakati ambapo uchambuzi wa uhakika zaidi wa vinasaba ulianza kuwa jambo la kawaida katika idara ya FBI.

Katika jumla ya kesi 268 zilizopitiwa upya mwezi uliopita na ambazo awali ushahidi wa uchambuzi wa nywele ulishatumika dhidi ya washitakiwa, asilimia 95 kati yao zilithibitika kuwa na ushahidi wa uliokosewa.

FBI yakiri kuwepo makosa

Naibu mkurugenzi mtendaji wa FBI, Amy Hess, amekiri kwamba, wataalamu 26 kati ya 28 wa idara hiyo ya upelelezi waligundulika aidha kutoa ushahidi uliokosewa au kuwasilisha ripoti za kimaabara zenye makosa. Hess ameongeza kuwa idara yake kwa kushirikiana na wizara ya sheria imewekeza rasilimali za kutosha kuhakikisha kuwa kesi zote zilizohusisha ushahidi wa uchambuzi wa nywele zinahakikiwa upya.

Michoro ya washukiwa wakiwa mahakamani.
Michoro ya washukiwa wakiwa mahakamani.Picha: Reuters/Rosenberg

Ingawa kuwepo kwa makosa kwenye ushahidi si lazima kumaanishe kuwa mshukiwa hana hatia, lakini watetezi wa sheria wanasema wanashirikiana na wizara ya sheria kuhakikisha kuwa washukiwa waliohukumiwa kwa ushahidi huo wanapata nafasi ya kukatia rufaa hukumu dhidi yao.

Tayari wizara ya sheria imeshasema kuwa haitaweka kizuizi chochote pindi watuhuniwa wa kesi kama hizo katika ngazi ya serikali kuu wataomba kesi zao kusikilizwa upya. Sehemu kubwa ya kesi hizo, hata hivyo, ziko kwenye kiwango cha serikali za majimbo, ambako FBI huwapa mafunzo maelfu ya wataalamu wa nywele kila mwaka.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman