1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maktaba ya muziki wa Kiafrika chuoni Mainz

Lina Hoffmann20 Machi 2012

Watafiti wa masuala ya makabila na tamaduni wa chuo kikuu cha Mainz hapa Ujerumani wamejenga maktaba ya miziki kutoka barani Afrika. Maktaba hiyo ilianzishwa miaka 20 iliyopita.

https://p.dw.com/p/14OGn
Chuo kikuu mainz Bilder aus dem Archiv für die Musik Afrikas (AMA) der Universität Mainz, undatiert, eingestellt im März 2012
Chuo kikuu mainzPicha: Janika Herz

Kitengo cha masuala ya makabila, tamaduni na masuala ya Afrika cha chuo kikuu cha Mainz kina ghala iliyo chini ya ardhi. Ghala hiyo ndiyo inayohifadhi maktaba ya muziki chungunzima kutoka barani Afrika.

Mkusanyiko huu ni wa kipekee kabisa hapa Ujerumani. Upo muziki wa aina ya Soul, Reggae, Highlife, Hip Hop, Jazz na hasa muziki aina ya Pop. Muziki huo unatoka katika nchi zilizomo kusini mwa jangwa la Sahara. Maktaba ya chuo kikuu cha Mainz haina nyimbo za zamani tu,ambazo hata huko Afrika zilikotokea hazipatikani tena kwa sasa, bali hata nyimbo mpya kama ulioimbwa mwaka 2011 na mwanamuziki Fatoumata Diawara kutoka Mali.

Maktaba hii ya muziki ina vyumba vitano ambamo sahani za santuri, kaseti, CD, mikanda ya video pamoja na DVD zimehifadhiwa na kupangwa kulingana na nchi au eneo ambapo muziki husika unatokea. Mtafiti wa masuala ya makabila na tamaduni, Bw. Wolfgang Bender, alianza kukusanya muziki wa Kiafrika mwaka 1991. Katika miaka iliyofuata aliendelea kununua muziki na wakati mwingine alizawadiwa kaseti zenye nyimbo kutoka Afrika. Watafiti wengi waliokuwa wakifanya kazi katika nchi za Afrika walimletea muziki kutoka katika nchi hizo.

Hauke Dorsch ni msimamizi wa maktaba ya muziki wa Kiafrika
Hauke Dorsch ni msimamizi wa maktaba ya muziki wa KiafrikaPicha: DW

Radio France International yatoa mchango

Kwa miaka miwili sasa, Hauke Dorsch ambaye pia ni mtafiti wa masuala ya makabila na tamaduni, amekuwa msimamizi wa maktaba ya muziki wa Kiafrika hapa Ujerumani. Kabla ya hapo, Dorsch alifanya utafiti juu ya kundi la wanamuziki na watungaji wa mashairi kutoka Afrika ya Magharibi wanaojulikana kama Griots. Dorsch anakumbuka hali ilivyokuwa wakati maktaba ilipokuwa ikianzishwa:

„Tulipiga hatua kubwa pale ambapo mwanzilishi Bender alipoleta mkusanyiko wa miziki kutoka Radio France International," anaeleza Dorsch. " Lakini jambo hili lilitokea baadaye sana, baada ya Radio France International kuamua kutumia mfumo wa digitali na kuacha kabisa kutumia muziki kutoka katika sahani za santuri. Huu ndio ulikuwa wakati ambapo maktaba yetu ilikua kwa kasi."

Muziki kutoka Tanzania, Kenya na Ghana

Nyimbo za zamani kuliko zote katika maktaba ya chuo kikuu cha Mainz ni za miaka ya 1940. Sehemu kubwa ya nyimbo hizo zinatoka Ghana, Kenya na Tanzania. Miongoni mwao zipo nyimbo za kwaya ya Kitanzania kutoka jijini Dar es Salaam inayoimba kwa kiswahili.

Muziki katika maktaba maalum ya chuo kikuu cha Mainz
Muziki katika maktaba maalum ya chuo kikuu cha MainzPicha: Hauke Dorsch

Lakini maktaba hii ya muziki haihifadhi tu nyimbo za wanamuziki kutoka Afrika. Pia zipo sauti na nyimbo mbalimbali zilizorekodiwa na watafiti wa masuala ya makabila na tamaduni wakati wakiwa katika safari zao za utafiti.

Wanafunzi wa chuo kikuu cha Mainz wanaweza kufanya utafiti katika maktaba yao. Msimamizi wa maktaba hiyo, Hauke Dorsch, hutoa semina kuhusu muziki, fasihi na filamu kutoka Afrika. Lakini maktaba hiyo vile vile inaweza kutumiwa na watu ambao si wanafunzi wa chuo kikuu. Hivyo kila mtu anaweza kufika hapo na kusikiliza muziki kutoka barani Afrika. Mara kwa mara wanachuo huandaa tamasha na maonyesho ya muziki huo.

Mwandishi: Ann-Kathrin Friedrichs

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman