1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano Honduras

Kabogo Grace Patricia30 Oktoba 2009

Honduras yafikia makubaliano ya kumaliza mzozo wa kisiasa

https://p.dw.com/p/KJ8F
Rais wa mpito wa Honduras Roberto MichelettiPicha: AP

Kufuatia shinikizo la kimataifa, serikali iliyoko madarakani nchini Honduras imekubali kumrejesha madarakani Rais Manuel Zelaya aliyeondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo miezi minne iliyopita. Hatua hiyo ilibainika jana Alhamisi baada ya Rais wa mpito, Roberto Micheletti kuwaamuru wapatanishi wake kusaini makubaliano ambayo yanaweza kumrejesha madarakani Bwana Zelaya, ingawa amesema uamuzi wa kuridhia makubaliano hayo uko mikononi mwa Mahakama Kuu na Bunge la nchi hiyo.

Micheletti amesema makubaliano hayo yaliyosainiwa hii leo, yataunda serikali ya kugawana madaraka na kuzitaka pande zote zinazohasimiana kutambua uchaguzi wa rais wa tarehe 29, ya mwezi ujao wa Novemba, hivyo kumaliza mzozo wa kisiasa uliokuwepo tangu mwezi Juni, mwaka huu. Bwana Micheletti amesema makubaliano hayo yataunda tume ya kuchunguza matukio ya miezi michache iliyopita, na ataziomba serikali za kigeni kuziangalia upya hatua ilizochukua kama vile kusimamisha misaada yake kwa Honduras na kufuta visa za viongozi wa serikali iliyoko madarakani.

Micheleti, alichukua madaraka ya Honduras, saa chache baada ya Zelaya kupinduliwa madarakani Juni 28, mwaka huu, na kulazimishwa kwenda kuishi uhamishoni kabla ya kurejea nchini Honduras mwezi uliopita na kupatiwa hifadhi na ubalozi wa Brazil uliopo Tegucigalpa huku majeshi ya nchi hiyo yakiuzingira ubalozi huo. Kwa wakati wote huo, Micheletti amekuwa akikataa kumrejesha madarakani Zelaya.

Jumuiya ya kimataifa

Marekani, Umoja wa Ulaya na viongozi wa Latin America wamekuwa wakisisitiza Zelaya arejee madarakani ili amalizie kipindi chake kinachokwisha mwezi Januari, mwaka ujao. Viongozi hao walitishia kutomtambua mshindi wa uchaguzi wa Novemba hadi demokrasia itakaporejeshwa nchini Honduras. Rais Barack Obama wa Marekani alisimamisha baadhi ya misaada kwa Honduras kufuatia mapinduzi hayo. Aidha, kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton aliamua kupeleka ujumbe kushinikiza kupatikana kwa makubaliano. Ujumbe huo ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Tom Shannon na Naibu Mjumbe Maalum wa Marekani katika nchi za Amerika Kaskazini na Kusini, Dan Restrepo, kabla walikutana kwa mazungumzo na kuonya kuwa muda wa kufikiwa makubaliano ulikuwa ukifikia ukingoni. Akizungumzia makubaliano hayo Shannon anasema:

''Sisi, na sio tu Marekani, lakini jumuiya yote ya Amerika imeanzisha mazungumzo haya kwa njia ambayo suluhisho linapatikana, na hivyo, kwa maoni yangu makubaliano ni makubaliano. Kile ambacho Wananchi wa Honduras wataka kukiamua miongoni mwao wenyewe, sisi tutakikubali.''

Nchi hiyo inayolima kahawa imekuwa ikitengwa kidiplomasia tangu Zelaya alipoondolewa madarakani. Zelaya aliwakasirisha wananchi wengi wa Honduras kwa kuwa mshirika wa Rais Hugo Chavez wa Venezuela. Wakosoaji wanasema pia Zelaya alikuwa akitaka kuungwa mkono kuongeza muda wake madarakani, madai ambayo ameyakanusha.

Pongezi

Wakati huo huo, Bibi Clinton, amepongeza makubaliano hayo ya kihistoria yenye lengo la kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Honduras na kufungua njia kuelekea kwenye uchaguzi wa rais.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AP)

Mhariri:Miraji, Othman