1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano Kuhusu Mradi wa Kinuklea wa Iran Magazetini

25 Novemba 2013

Makubaliano ya muda kuhusu mpango wa kinuklea wa Iran ,mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi mjini Warsaw na mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1ANW7
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akizungumzsa na waandishi habari baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano mjini GenevaPicha: Reuters

Tuanzie lakini na makubaliano yaliyofikiwa Geneva.Katika wakati ambapo nchi za magharibi zinayasifu makubaliano hayo na kuyataja kuwa hatua ya kwanza muhimu kulekea makubaliano timamu,Israel na baadhi ya nchi za kiarabu zinayatia ila.Gazeti la "Darmstädter Echo" linaandika:"Kwa miaka Israel iliweza kutegemea katika mgogoro wa mradi wa kinuklea wa Iran,kuwa Marekani itapinga tu aina yoyote ya maridhiano.Hayo yamepita sasa na wa kulaumiwa ni Netanyahu na serikali yake.Siasa yake shupavu ya ujenzi wa makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi katika maeneo ya ukingo wa magharibi wa mto Jordan imevuruga uwezekano wa kufikiwa makubaliano pamoja na wapalastina-makubaliano ambayo yamemkaa sana rohoni rais wa Marekani Barack Obama.Madhara ya ukakamavu anayaona hivi sasa Netanyahu:Hakuna yeyote anaesikiliza onyo lake dhidi ya bomu la Iran,hata ikulu ya Marekani haimsikilizi."

Mhariri wa gazeti la "Donaukurier anakwenda mbali zaidi anaposema:"Makubaliano ya Geneva ni ushindi mkubwa kwa uongozi mpya wa Iran.Hata miezi minne haijakamilika tangu rais Hassan Ruhani aingie madarakani,wawakilishi wake wameketi pamoja na wale wa jumuia ya kimataifa na kujadiliana uso kwa uso kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran.Iran sasa inabidi idhihirishe kwamba haidhamirii kuvuta wakati na inabidi pia ijitolee zaidi ili makubaliano timamu yaweze kufikiwa kwa muda uliopangwa.Bila shaka Ruhani atalazimika kuvumilia vishindo nyumbani.Tayari kuna wanaomtuhumu kuyaendea kinyume masilahi ya taifa.

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi haujafana

Mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi mjini Warsaw nao pia umezingatiwa.Mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau"anahisi:"Mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi umeshindwa.Ufumbuzi uliopatikana na ambao haustahiki kuitwa hivyo,ni ushahidi wa kushindikana mazungumzo ya Warsaw.Wote wanasikia onyo linalotolewa na watafiti wa tabia nchi.Lakini hakuna yeyote anaetaka kufanya chochote."

Siku tatu kukamilisha mazungumzo ya kuunda serikali Berlin

Mada yetu ya mwisho magazetini hii leo inatufikisha mjini Berlin ambako wahariri wa magazeti wametupia jicho juhudi za kukamilisha kwa wakati mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano kati ya vyama vya Christian Democratic Union CDU,Christian Social Union CSU na wana Social Democratic wa SPD.Gazeti la "Saarbrücker Zeitung " linaandika:"Katika kipindi cha wiki sabaa zilizopita washiriki katika meza ya mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano wamezama katika bahari nani anataka nini.Vipi watafanikiwa hadi jumatano ijayo kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya muungano itakayoleta mageuzi ya maana,hata wenyewe wanaozungumza hawajui.Bora zaidi ingekuwa kama Merkel,Seehofer na Gabriel wangevua majokho ya vyama na kuuangalia muungano wa vyama vikuu kama ulivyo yaani fursa ya maana ya kupitisha mageuzi yanayohitajika kwa mustakbal wa nchi hii.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu