1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani ya Jamhuri ya Afrika kati Magazetini

Oumilkheir Hamidou
23 Juni 2017

Makubaliano ya amani katika jamhuri ya Afrika kati, na wanubi waliochoshwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la Nuba kati ya Sudan kusini na Sudan ni miongoni mwa mada za Afrika Magazetini

https://p.dw.com/p/2fG6s
Zentralafrikanische Republik Charles Armel Doubane und Armel Mingatoloum Sayo
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Stinellis

Tunaanzia mjini Roma nchini Italia yalikotiwa saini wiki hii makubaliano ya amani kati ya pande zinazopigana vita katika jamhuri ya Afrika kati. Ripoti ya gazeti la mjini Münich, Süddeutsche  iliyopewa kichwa cha maneno "Waraka kwaajili ya Amani" inazungumzia jinsi wawakilishi wa serikali na makundi ya waasi wa nchi hiyo walivyotia saini makubaliano hayo ya amani mjini Roma. Chini ya upatanishi wa Ushirika wa Sant'Egidio, vuguvugu la kikatoliki linalopigania amani na haki za binaadam kote ulimwenguni, serikali ya jamhuri ya Afrika kati na wawakilishi wa makundi ya wanamgambo nchini humo wamekubaliana jumatatu usiku mjini Roma kuweka chini silaha mara moja , makubaliano yatakayosimamiwa na jumuia ya kimataifa. Süddeutsche linakumbusha  chanzo cha kuripuka vita hivyo  msimu wa kiangazi mwaka 2013  na kuangamiza maisha ya maelefu ya watu , wengi kati yao ni raia wasiokuwa na hatia.

Makubalianao ya leo hayana tofauti na yaliyopita

Licha ya kuchaguliwa serikali mpya  inayoongozwa na rais Faustin Touadéra na vikosi vya Ufaransa kuihama nchi hiyo, amani haijapatikana. Serikali inadhibiti eneo la mji mkuu tuu  huku wanajeshi wa Umoja wa mataifa wakifanikiwa kuhakikisha usalama katika miji mikubwa tu. Sehemu kubwa ya maeneo yanayozungukwa na misitu baado inadhibitiwa na makundi ya wanamgambo, linaandika gazeti la Süddeutsche linalotaraji makubaliano ya amani ya Roma yatasaidia kumaliza mivutano. Mbali na kuweka chini silaha, makubaliano hayo yanazungumzia pia juu ya kupokonywa silaha waasi pamoja na kujumuishwa katika vikosi vya jeshi au katika maisha ya kawaida ya jamii, kuundwa tume ya ukweli, haki na suluhu huku serikali ya mjini Bangui  ikiahidi kubatilisha vikwazo dhidi ya pande zinazohusika na mzozo huo. Süddeutsche linamaliza kwa kusema makubaliano ya Roma hayakuyapita makubaliano yaliyotangulia na hakuna ahadi iliyotolewa  ya kuwaachilia huru wanamgambo wanaoshikiliwa.

Wanubi wamechoshwa na vita

Nchi nyengine inayosumbuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ni Sudan ambayo gazeti la Neues Deutschland linasema wanubi wameshachoshwa na vita hivyo ambavyo gazeti linasema vimeripuka tangu miaka ya 80 katika maeneo ya milimani kati ya Sudan Kusini na Sudan. Kufuatia mwongozo mpya wa Sudan,eneo la Nuba likajumuishwa sehemu ya kaskazini. Tangu Sudan Kusini ilipoamua kujitenga mwaka 2011, mapigano yameripuka upya. Neues Deutschland linazungumzia shida za kila aina wanazokabiliana nazo watumishi wa mashirika ya misaada ya kiutu wanapotaka kusafirisha misaada hadi katika maeneo hayo ya milimani. Mashirika ya misaada ya kiutu na waandishi habari wamepigwa marufuku na serikali ya mjini Khartoum kuingia katika maeneo hayo.

 

Shirika la Ujerumani la  misaada ya kiutu la Cap Anamur liaendesha shughuli zake katika eneo hilo kutokana na ruhusa ya kundi la waasi la Jeshi la ukombozi wa Sudan kaskazini-SPLA-N wanaolidhibhiti eneo la Nuba."Huku hakuna njia, kuna magari kati ya 40 na 50 tu" amenukulia Johannes Plate wa shirika la Cap Anamur akisema. Plate na mwenzake Rene Hildenbrandt wanalazimika kuchukua madawa toka Sudan Kusini kuyapeleka katika eneo hilo la milimani wanakoishi watu kati ya laki nane na milioni moja na laki mbili. Sio tu hakuna njia, katika eneo la milimani la Nuba hakuna umeme, hakuna maji safi ya kunywa wala mfumo wa mawasiliano. Hakuna maendeleo wala vitega uchumi na hiyo ndio sababu ya ugonvi linasema Neues Deutschlad."Tunapigana kwaajili ya kudai umoja, haki na uhuru, tunabaguliwa na serikali ya Khartoum.Tunataka kuwa sawa na nchi yoyote ile ya dunia....Khartoum ikitekeleza masharti hao, tunataka kuwa na Sudan iliyoungana" amenukuliwa  jenerali Hamza  wa wanamgambo wa SPLA-N akisema.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri:Yusuf Saumu