1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya Ushirikiano wa Uchumi yahofiwa

P.Martin24 Mei 2007

Wanaharakati wanaopiga vita umasikini wamelinganisha majadiliano ya biashara kati ya Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Kiafrika sawa na mchezo wa ndondi kati ya mwanafunzi na bingwa wa uzito wa juu.

https://p.dw.com/p/CHkp
Wakulima wa kahawa nchini Ethiopia
Wakulima wa kahawa nchini EthiopiaPicha: AP Photo

Hitilafu kama hiyo hasa hudhihirika katika mazungumzo yanayofanywa na Umoja wa Ulaya pamoja na serikali za nchi za Afrika ya Mashariki na za kusini mwa bara hilo.Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwaka huu,ungependelea kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kwa ufupi EPA.

Miongoni mwa wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya,mataifa 4 ni kutoka kundi la madola tajiri kabisa yalioendelea kiviwanda yaani G-8.Upande wa pili kutoka jumla ya mataifa 16 yanayoshiriki katika mazungumzo hayo,13 yametambuliwa na Umoja wa Mataifa kama ni nchi zilizo masikini kabisa duniani.

Hivi karibuni,Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya,Peter Mandelson alisema,umoja huo utafungua masoko yake kwa bidhaa zinazotoka Afrika kuanzia siku ya mwanzo ya kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi.Vile vile nchi za Kiafrika zitaruhusiwa kipindi kirefu cha mpito kuondosha vikwazo vyake dhidi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka Ulaya.

Lakini uchunguzi mpya uliofanywa na mashirika matatu ya misaada yamesema,hatimae nchi za Kiafrika zitapaswa kufuta ushuru wa forodha kwa asilimia 80 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya.Hatua hiyo itazinyima nchi za Kiafrika pato muhimu,kwani asilimia 25 ya mapato yao hutegemea ushuru wa forodha.Zambia kwa mfano itapoteza takriban dola milioni 16,ikiwa ni sawa na bajeti yake ya kila mwaka kupiga vita UKIMWI.

Wasiwasi kuhusu Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi,yanayotarajiwa kutiwa saini kati ya Umoja wa Ulaya na nchi 16 za Afrika ya Mashariki na Kusini mwa Afrika,umeelezwa pia na Mtandao wa Haki za Kiuchumi nchini Malawi.Temwa Gondwe wa mtandao huo,anahofia kuwa Malawi huenda ikauza nchi za nje mazao yake ya tumbaku,chai na kahawa bila ya bidhaa hizo kutengenezwa tayari kwa matumizi.Akasema,kinachohitajiwa ni utaratibu wa kuongeza thamani ya bidhaa hizo ili mazao hayo yaweze kusafirishwa kama bidhaa zilizokamilika kutengenezwa.Lakini masharti ya kutia saini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi hayadhamini kuwa kutakuwepo utaratibu wa aina hiyo.Gondwe anabashiri kuwa serikali ya Malawi huenda ikakubali mkataba usio na hali nzuri hivyo,ikihofia kuwa kukataa kwake kutia saini, huenda kukasababisha Umoja wa Ulaya kulipiza kisasi kwa kuzuia misaada yake kwa Malawi. Akaongezea kuwa bajeti ya Malawi inategemea sana kusaidiwa kutoka nje na isingependa kuonekana ikienda kinyume na wafadhili wake.

Hata nchini Kenya wanaharakati wa shirika linalopigania biashara ya haki wanasema,mikataba ya EPA itamaanisha maafa kwa wakulima wa nchi hiyo.Hofu yao ni kwamba wakulima hao watajikuta wakishindana na bidhaa nyingi kutoka Ulaya kama vile mazao ya maziwa,mahindi,ngano,nafaka na nyama-mazao ambayo hupata msaada mkubwa wa pesa kutoka serikali zao.

Lawama moja kuu inayoikabili sera ya kilimo ya Umoja wa Ulaya ni kwamba inawaumiza wakulima katika nchi masikini kwa kuyajaza masoko yao na bidhaa rahisi kutoka Ulaya wakati ambapo wakulima wa nchi zilizo masikini hawana hata uwezo wa kushindana na bidhaa hizo.