1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano yafikiwa kuingiza misaada ya kiutu Homs

7 Februari 2014

Syria na Umoja wa mataifa zimefikia makubaliano kwa maeneo yaliyozingirwa ya mji wa Homs,na mashirika ya kijamii yamesema watu 250 wameuwawa katika mashambulio ya jeshi likitumia mabomu ya mapipa huko Aleppo.

https://p.dw.com/p/1B4b9
Krieg in Syrien Homs 25.01.2014
Mji wa Homs umebakia magofuPicha: Reuters

Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeitaka Syria kuharakisha uondoaji wa silaha zake hatari za sumu ili kufikia muda uliowekwa wa Juni 30 mwaka huu wa kukamilisha zoezi hilo la kuharibu silaha hizo.

TaaUmoja wa Mataifa umetangaza kuwa kutakuwa na usitishaji wa muda wa mapigano ikiwa ni "hatua ya kibinadamu", na msemaji wa katibu mkuu Ban Ki-moon , Farhan Haq alisema hayo kwa kumnukuu katibu mkuu msaidizi anayehusika na masuala ya kiutu na misaada ya dharura Valerie Amos.

Homs Syrien Zerstörung Verwüstung Krieg
Magofu katika mji wa HomsPicha: Reuters

Makubaliano hayo yanasafisha njia kuwezesha upelekaji wa mahitaji yatakayoweza kuokoa maisha kwa raia wanaofikia kiasi ya 2,500, huku wanaharakati wakisema watu wamekuwa wakiishi wakiwa na vitu vichache tu kwa wiki kadha.

Baada ya majadiliano

Wiki moja baada ya hali ya wilaya iliyozingirwa ya mji wa Homs kujadiliwa katika mazungumzo ya amani mjini Geneva , shirika la habari la taifa nchini Syria SANA, limesema makubaliano yamefikiwa kuruhusu misaada pamoja na eneo la kupita raia kwa usalama.

"Gavana wa Homs Talal al-Barazi na mratibu wa Umoja wa Mataifa Yaacoub El Hillo wamefikia makubaliano ya kupata njia ya kupita kwa raia wasio na hatia kutoka mji huo mkongwe na kuingia kwa msaada wa kiutu kwa raia ambao wataamua kubakia katika eneo hilo," shirika hilo limesema.

Shirika hilo la habari SANA, limeongeza kuwa " maafisa wahusika wa Syria watatekeleza makubaliano hayo kwa kutoa msaada unaohitajika wa kiutu".

Valerie Amos UN Nothilfekoordinatorin
Mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa mataifa Valerie AmosPicha: picture-alliance/dpa

Wilaya inayodhibitiwa na waasi katika mji wa Homs imekuwa ikishambuliwa karibu kila siku tangu jeshi lilipowazuwia Juni mwaka 2012.

Miongoni mwa wakaazi waliozingirwa ni pamoja na kiasi ya wanawake 1,200, watoto na wazee, limesema shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu mjini London.Msemaji wa kamisheni ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa Jens Laerke amesema kuwa misaada iko tayari.

"Umoja wa Mataifa na washirikawake wa masuala ya kiutu wameweka chakula, dawa na mahitaji mengine nje ya mji wa Homs, tayari kuweza kusambazwa mara itakapotolewa ruhusa na pande zinazohusika kuingia kwa usalama."

Shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria limesema wakati huo huo kuwa , zaidi ya watu 250 wameuwawa katika siku sita za mashambulio ya jeshi la serikali dhidi ya mjini wa Aleppo , ambapo muungano wa waasi umetangaza operesheni mpya ya kijeshi katika jimbo hilo.

Pia katika eneo la kaskazini mwa Syria , mapambano yametokea baina ya waasi na jeshi la serikali katika jela katikati ya mji wa Aleppo, baada ya wapiganaji wa makundi ya Kiislamu kushambulia jela hiyo na kuwaacha huru mamia ya wafungwa, limesema shirika hilo la kuangalia haki za binadamu nchini Syria.

Operesheni mpya

Kundi la Jeshi la Waislamu, ambalo linajumuisha maelfu ya wapiganaji , pamoja na kundi lenye mafungamano na al-Qaeda la Al-Nusra yametangaza operesheni ya pamoja inayojulikana kama "mtazamo wa ahadi ya ukweli", ikiwa ni kwa mujibu wa aya katika kitabu cha Koran.

Tangazo hilo limekuja wakati jeshi ya serikali linataka kuchukua maeneo katika eneo linalodhibitiwa na waasi la mashariki ya mji wa Aleppo.

Jens Laerke
Msemaji wa ofisi ya uratibu wa misaada ya dharura ya Umoja wa mataifa, jens LaerkePicha: DW

Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka serikali ya Syria kuchukua hatua za haraka ili kutimiza majukumu yake, rais wa baraza hilo kwa mwezi huu balozi wa Lithuania katika umoja wa Mataifa Raimonda Murmokaite amewaambia waandishi habari.

Silaha za sumu zinahitajika kusafirishwa hadi katika bandari ya Latakia , katika utaratibu na hatua za haraka, Murmokaite amesisitiza, baada ya kutoa mukhtasari wa majadiliano ya faragha katika baraza hilo mapema jana Alhamis, pamoja na Sigrid Kaag, ambaye amepewa jukumu la uratibu katika kuangamiza silaha hizo.

Mwandishi: Sekione kitojo / afpe

Mhariri: Josephat Charo