1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makumbusho ya Chai Norddeich

17 Novemba 2015

Makumbusho ya maisha ya kale ni sehemu ya maisha na utamaduni wa wajerumani na jamii nyingine nyingi za Ulaya. Yapo makumbusho ya aina mbali mbali, yakiwemo ya vyakula na vinywaji kama vile chai.

https://p.dw.com/p/1H7QN
Tee-Museum in Norddeich
Vyombo vya kuandalia chai vilivyotumiwa eneo la Frisialand miaka ya nyumaPicha: DW/D. Gakuba

Katika mji mdogo wa Norddeich ulio Kaskazini Magharibi mwa Ujerumani, kuna makumbusho ya kinywaji cha chai ambacho ni maarufu sana katika eneo hilo la Frisialand, ambako ni chimbuko la ng'ombe wa kisasa wanaoenea kwa kasi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, kutokana na uwezo wao wa kutoa maziwa mengi.

Hivi karibuni niliutembelea mji huo, nikapata kuyatembelea makumbusho hayo, na kukuta watalii wengi waliofika kujionea wenyewe historia ya chai na namna ilivyonywewa miaka zaidi ya mia mbili iliyopita. Kwa msaada wa mkurugenzi wa makumbusho hayo, Bi Anke Zimmer, nilifahamishwa kila kitu kinachoendana na utamaduni wa chai katika eneo hilo.

Tee-Museum in Norddeich
Bi Anke Zimmer katika jiko la kizamani kwenye makumbushoPicha: DW/D. Gakuba

Umasikini ulikuwa hali ya kawaida

Nilivutiwa na kuona katika maonyesho hayo jinsi mazingira ya jiko la wajerumani wakati huo, yalivyo sawa na yale unayoyakuta katika nyumba nyingi vijijini kwetu Afrika Mashariki.

Hali kadhalika nilivutiwa na kufahamishwa kwamba desturi nyingi zinazoambatana na unywaji chai wakati huo, zina uhusiano na uhaba wa chakula, ambao ulikuwa tatizo sugu barani Ulaya enzi hizo za zamani kidogo. Hiyo inaondoa dhana iliyokita mizizi katika mawazo ya waafrika wengi, wanaodhani kwamba tangu jadi nchi za wazungu zilikuwa matajiri.

Je, twaweza kuiga mfano huo?

Bada ya ziara kwenye makumbusho hayo, nilijiuliza ikiwa haifai hata sisi huko kwetu Afrika kutunza kumbukumbu ya utaratibu wetu wa maisha ya kila siku! Hatuwezi kuweka makumbusho ya namna vinywaji kwama Lubisi huko Kagera, Mbege maeneo ya Kilimanjaro na aina nyingine mbali mbali za pombe ya kienyeji zilivyokuwa zikitengenezwa ili watoto wetu na wajukuu wenye shauku ya kujua chimbuko lao waweze kuviona.

Kujua zaidi unaweza kusikiliza makala ya Sura ya Ujerumani kuhusu makumbusho hayo, ukibonyesha alama ya kipaza sauti cha masikioni hapo chini.

Daniel Gakuba

DW-Kiswahili