1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya kisiasa yafikia maridhiano

Saumu Mwasimba27 Agosti 2007

Makundi ya kishia, sunni na wakurdi yametia saini mpango wa maridhiano utakaojenga upya mpango mzima wa kisiasa Iraq.

https://p.dw.com/p/CB1j
Picha: AP

Waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki amesema viongozi wa makundi ya kishia,Sunni na wakurdi wametia saini mpango wa maridhiano.

Kwa mujibu wa bwana Maliki Mapatano hayo ni hatua yapili ya kuelekea kujenga upya mpango wa kisiasa baada ya vyama vya washia na wakurdi kuunda muungano mpya.

Viongozi hao wamekubaliana kulegeza masharti dhidi ya wanachama wa zamani wa chama cha aliyekuwa kiongozi wa Iraq Saddam Hussein cha Baath kujiunga na serikali, kufanyika uchaguzi wa mikoa jambo ambalo limependekezwa zaidi na Marekani pamoja na kusaidia vikosi vya usalama kukomesha umwagikaji wa damu.

Hatua hiyo iliyofikiwa hapo jana imeungwa mkono na Marekani ambayo imesema ni dalili muhimu katika kuleta umoja nchini Iraq.

Waziri mkuu al Maliki amekuwa akikosolewa na wanasiasa wa Marekani katika siku za hivi karibuni.

Hata hivyo hapo jana al Maliki aliwashutumu wanasiasa wa Marekani Hillary Clinton na Carl Levin ambao waliitaka serikali ya Iraq imuondoe uongozini akisema wanasiasa hao wanaichukulia Iraq kama ni mali yao wanapaswa kuheshimu demokrasia.