1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malengo ya maendeleo ya Milenia.

Abdu Said Mtullya22 Septemba 2010

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema harakati za kupambana na umasikini zinaweza kurudi nyuma ikiwa misaada ya maendeleo haitadhibitiwa.

https://p.dw.com/p/PInf
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akihutubia kwenye Umoja wa Mataifa.Picha: AP

NEW YORK:

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametahadharisha juu ya uwezekano wa kurudi nyuma kwa kiwango kikubwa kattika harakati za kupambana na umaskini duniani ikiwa masharti thabiti hayataambatanishwa na misaada ya maendeleo.

Kansela Merkel ametoa tahadhari hiyo katika hotuba yake kwenye mkutano maalumu wa Umoja wa Mataifa, juu ya malengo ya maendeleo ya Milenia.

Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali kutoka duniani kote, wanaohudhuria mkutano huo wanatathmini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa malengo hayo.

Katika hotuba yake bibi Merkel pia amesisitiza umuhimu wa kuigharamia miradi ya maendeleo itakayoleta mafanikio katika nchi maskini.Pia amezitaka nchi hizo ziache kutegemea kupewa misaada daima, na badala yake ziwajibike zenyewe katika kuleta maendeleo yao na zihakikishe kwamba zinatumia vizuri raslimali zao.

Kiongozi wa Ujerumani amesema nchi yake inayotoa mchango mkubwa wa fedha kwenye Umoja wa Mataifa kuliko nyingine zote, inajitahidi ili ifikie lengo la kutenga asilimia 0.7 ya pato lake jumla kwa ajili ya misaada ya maendeleo. Mnamo mwaka huu mchango wa Ujerumani ni asilimia 0.4 ya pato lake jumla la ndani.