1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malengo ya milenia yatafikiwa kutokana na upatikanaji bora wa maji

Sekione Kitojo10 Septemba 2010

Uendeshaji na upatikanaji wa vyanzo vya maji , huduma za maji na usalama wa maji ni njia bora zaidi za matumizi mazuri ya maji ili kuweza kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya milenia.

https://p.dw.com/p/P9QN
Rita R. Colwell, kutoka Marekani akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa maji duniani mjini Stockholm, Sweden.Picha: AP

Uendeshaji na upatikanaji wa vyanzo vya maji , huduma za maji na usalama wa maji ni njia bora zaidi za matumizi mazuri ya maji ili kuweza kuangalia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya milenia. Ni ukweli kwamba malengo ya maendeleo ya milenia yatafikiwa kwa matumizi mazuri ya maliasili hiyo na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na usafi. Hayo yamezungumzwa na wataalamu wa maji katika kikao cha leo cha wiki ya maji duniani mjini Stockholm wakati wakijadili malengo ya maendeleo ya milenia kuhusiana na maji.

Matumizi ya kutosha ya utaalamu uliopo hivi sasa utapunguza mateso ya mamilioni ya watoto , wanawake na wanaume. Pia yatafungua njia kwa matumizi mazuri ya nguvu kazi ya watu pamoja na fedha katika kufikia changamozo nyingine za maendeleo. Lakini mahitaji ya maji yanahitaji kuangaliwa zaidi katika masuala ya kisera, uwekezaji na uendeshaji. Hali ya kuendelea kupuuzia italeta maafa , na kushindwa kwa malengo yote ya maendelea ya milenia.

Juhudi za kutatua mzozo wa dunia wa maji zinavurugwa hata hivyo kwa kiasi kikubwa na utawala mbovu, rushwa, unyang'anyi , ubadhirifu na kiwango cha juu cha ufisadi. Rushwa katika sekta ya maji ni sababu kuu na kishawishi kikuu cha mzozo wa maji duniani ambao unatishia maisha ya mabilioni ya watu na kuongeza kasi ya uharibifu wa mazingira. Hayo yamelezwa na kituo kinachohimiza uadilifu katika matumizi ya maji cha mjini Berlin kilichoanzishwa mwaka 2006.

Ukosefu wa maji safi unawafanya watu kuwa masikini. Ukosefu wa maji ya kutosha pamoja na hali ya usafi inawanyima mabilioni ya watu, hususan wanawake na wasichana , fursa, heshima, usalama na hali bora.

Na tafiti kadha katika nchi mbali mbali , ikiwa ni pamoja na Indonesia, Bolivia , Lesotho, Chile, Kazakhstan na Uganda , zinathibitisha kuwapo na utawala mbovu katika sekta ya maji.

Akiulizwa iwapo ubadhirifu umepungua ama kuongezeka katika sekta ya maji tangu mwaka 2006, Hakan Troop, mwenyekiti wa taasisi hiyo ameliambia shirika la habari la IPS kuwa ni vigumu kusema iwapo ufisadi umeongezeka ama umepungua katika muda wa miaka ya hivi karibuni. Hatuna kipimo cha kulinganisha , na kiwango cha uwazi kuhusiana na uwekezaji katika sekta ya maji uko chini mno amelalamika.

Lakini kile ambacho kimekuwa cha manufaa ni kwamba sera za kupambana na rushwa hivi sasa ziko imara zaidi katika agenda ya maendeleo ya sekta ya maji duniani kote.

Kikao kilichojadili kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia kuhusiana na maji mjini Stockholm , kimesisitiza kuwa maji safi na salama ni miongoni mwa hatua muhimu sana za uzuwiaji wa vifo vya watoto. Upatikana wa maji unazuwia magonjwa na uambukizaji ambao unaathiri afya ya mama mjamzito na kuchangia katika vifo vya mama wajawazito wakati wa uzazi.

Kikao kicho cha wiki ya maji kinamalizika rasmi kesho tarehe 11.09.

Mwandishi : Sekione Kitojo / IPS / World Water Week web.

Mhariri : Othman Miraj.