1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMali

Mali yaitaka MINUSMA kuondoka nchini humo mara moja

Lilian Mtono
17 Juni 2023

Utawala wa kijeshi nchini Mali umeuagiza ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA kuondoka mara moja.

https://p.dw.com/p/4Si6i
Mali Verteidigungsminister Pistorius im Camp Castor
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Ombi hilo lililotolewa jana Ijumaa linaashiria kuzorota kabisa kwa uhusiano kati ya MINUSMA na serikali tangu utawala wa kijeshi ulipoingia madarakani mnamo 2020.

Utawala huo wa kijeshi nchini Mali umeongeza vizuizi dhidi ya operesheni za walinda amani, na hapo jana uliushutumu ujumbe huo kwa sio tu kushindwa kulinda amani, bali pia umekuwa sehemu ya tatizo lililopo nchini humo.

Soma pia: Ujerumani kuondosha wanajeshi wake Mali

Akijibu ombi hilo, mkuu wa jeshi la MINUSMA, linaotarajiwa kumaliza operesheni zake Juni 30, El Ghassim Wane amesema ulinzi wa amani huzingatia kanuni ya ridhaa kutoka kwa nchi mwenyeji na ikiwa ridhaa hiyo haitokuwepo, ni wazi kwamba operesheni hiyo haitawezekana.

Utawala huo tayari umekatisha ushirikiano wa muda mrefu na Ufaransa na washirika wengine wa Magharibi katika vita vyake dhidi ya makundi ya misimamo mikali, na kuigeukia Urusi kwa usaidizi wa kisiasa na kijeshi.