1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maliki ahusishwa na kutekwa kwa Mosul

16 Agosti 2015

Jopo la uchunguzi la bunge nchini Iraq limemhusisha waziri mkuu wa zamani Nuri al- Maliki na maafisa wengine 35 na kutekwa kwa mji wa Mosul na wapiganaji wa jihadi na kuweka uwezekano kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.

https://p.dw.com/p/1GGNQ
Wapiganaji wa Dola la Kiislamu walipouteka mji wa Mosul 2014.
Wapiganaji wa Dola la Kiislamu walipouteka mji wa Mosul 2014.Picha: picture-alliance/AP Photo

Wakati makamanda kadhaa waandamizi na viongozi wa kisiasa kwa muda mrefu wamekuwa wakionekana kuhusika na kutekwa kwa mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Iraq na wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu, repoti hiyo kwa mara ya kwanza imewataja kwa majina.

Mbunge ambaye ni mjumbe wa jopo hilo la uchunguzi Abdulrahman al-Shammari amesema kwamba Maliki ambaye alikuwa waziri mkuu kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka jana ni miongoni mwa wale waliotajwa.

Kujumuishwa kwa jina la Maliki ni chanzo cha utata kwa kamati hiyo ya bunge ambapo chama chake cha Dawa kimekuwa kikishinikiza kuundolewa kwa jina hilo.

Hatua za kisheria

Repoti hiyo ilioelezea kwa kina kile ilichokigunduwa katika uchunguzi wao ambao bado haukutangazwa hadharani imewasilishwa kwa spika wa bunge Salim al - Juburi ambaye amesema itapelekwa kwa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali kwa ajili ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.

Vikosi vya usalama vya Iraq.
Vikosi vya usalama vya Iraq.Picha: AFP/Getty Images/A. Shallal

Juburi amesema katika taarifa hakuna mtu alie juu ya sheria na kuhojiwa kwa watu hao kutapelekea mahakama kuwaadhibu wale waliohusika.

Kundi la Dola la Kiislam lilifanya shambulio lililosababisha maafa na uharibifu hapo tarehe tisa Juni mwaka jana na kuuteka mji wa Mosul siku iliyofuatia na halafu kuendelea kuteka maeneo mengi ya kaskazini na magharibi mwa mji mkuu wa Baghdad.

Vikosi mchanganyiko vya Iraq vilisambaratika wakati wa shambulio la awali kaskazini mwa nchi hiyo ambapo kuna wakati viliacha silaha zao pamoja na zana nyengine ambazo wapiganaji wa jihadi baadae walizitumia kuendeleza mapambano yao.

Maliki alipalilia mfarakano

Maliki kwa kiasi kikubwa anaonekana kuwa amepalilia mfarakano wa kimadhehebu kati ya Washia walio wengi nchini humo na Waarabu wa mdhehebu ya Sunni walio wachache.

Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq Nuri al-Maliki.
Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq Nuri al-Maliki.Picha: picture-alliance/AP Photo

Hali ya kutoridhika miongoni mwa Waarabu wengi wa madhehebu ya Sunni nchini humo ambao wanasema wanatengwa na serikali ya Maliki imetimiza dhima kuu katika kuifanya hali ya usalama kuzidi kuwa mbya nchini Iraq na hatimae kupelekea shambulio hilo la maafa la Dola la Kiislamu.

Maliki pia aliwateuwa makamanda chini ya misingi ya uaminifu wao kwake binafsi badala ya uwezo na alikuwa mkuu wa majeshi katika kipindi cha miaka miwili ambapo jeshi la Iraq halikufanya mazoezi yoyote yale muhimu jambo lililopelekea kushuka kwa umahiri wake.

Makamanda wa Ramadi kuwajibishwa

Mapema Jumapili ofisi ya Waziri Mkuu Haider al- Abadi imesema kiongozi huyo ameridhia kushtakiwa katika mahakama za kijeshi kwa makamanda waandamizi waliohusika na kuboronga kijeshi kwa hivi karibuni katika mji wa Ramadi mji ulioko magharibi ya Baghdad.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi.
Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi.Picha: Reuters/K. al-Mousily

Kundi la Dola la Kiislamu liliteka mji wa Ramadi hapo mwezi wa Mei baada ya vikosi vya serikali kuhimili mashambulizi ya wanamgambo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Taarifa ya ofisi yake hiyo imesema viongozi kadhaa wa kijeshi watashtakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa kutelekeza nafasi zao bila ya kuamuriwa kufanya hivyo na kinyume na maelekezo licha ya kuagizwa mara kadhaa wasiondoke.

Abadi awali alisema vikosi viliokuweko Ramadi vilitakiwa viwazuwiye wamgambo kuingia katika mji huo na kwamba ingelikuwa wamefanya hivyo wasingeliupoteza mji wa Ramadi.Afisa mwandamizi wa kijeshi wa Uingereza Brigedia Christopher Ghika amesema wameupoteza mji huo kwa sababu kamanda wa Iraq huko Ramadi aliamuwa kuondoka.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP

Mhariri : Sudi Mnette