1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester United na Arsenal kuonesha ubabe

Aboubakary Jumaa Liongo29 Aprili 2009

Katika viwanja vya spoti macho yote na masikio ya washabiki wa kabumbu duniani leo usiku kama yataelekezwa huko Uingereza katika nusufainali ya pili ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kati ya Arsenal na Manchester United.

https://p.dw.com/p/HgZo

Nusufainali ya kwanza ilifanyika hapo jana ambapo Chelsea na Barcelona zilitoka sare.


Katika pambano la leo ambalo litafanyika katika uwanja wa Old Trafford jijini Manchester, kocha wa Arsenal Arsene Wenger amepanga mikakati ya kupata angalau bao moja la ugenini, huku Sir Alex Ferguson akitaka kushinda bila ya mlango wake kuguswa.


Sir Ferguson amesema kuwa anatarajia kutumia mbinu za tahadhari ya juu kwa kuwabana sana wapinzani wao wasipate bao na wakati huo huo kupata ushindi ijapo mwembamba.


Kwa upande wake Arsene Wenger amesema kuwa atatumia mbinu za kushambulia zaidi ili kupata bao la ugenini na kwamba huu ni wakati wa kikosi chake chipukizi kuonesha makali yao.


Mara ya mwisho kwa timu hizo mbili kukutana ilikuwa kiasi cha wiki mbili zilizopita katika nusufainali ya kombe la FA ambapo Arsenal ilishinda kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka suluhu bin suluhu hata pale mpambano uliporefushwa.Hata hivyo Manchester United katika mechi hiyo iliteremsha takriban kikosi cha pili.


Ama katika nusufainali ya jana usiku huko Nuocamp uhispania, Barcelona pamoja na kutawala mchezo kwa muda mrefu ilishindwa kuipenya ngome ya Chelsea na hivyo kulazimishwa kutoka suluhu bi suluhu.


Fußball Arsene Wenger Sir Alex Ferguson
Arsene Wenger kulia na Sir Alex FergusonPicha: picture-alliance / dpa

Chelsea ilionekana kujihami zaidi na kuruhusu Barcelona kudhibiti mpira karibu muda mwingi wa mchezo huku Lionel Messi akionekana kuwa mwiba, ingawaje ufunguo wa kufungua mlango wa vijana hao wa London haukupatikana.


Kocha wa Chelsea Guus Hiddink alikiri kuwa walicheza chini ya kiwango


INSERT:HIDDINK


Hatukuweza kudhibiti mpira katika kipindi cha kwanza.Tulipoteza mipira mingi na kutoa nafasi kwa wapinzani wetu kufanya mashambulizi zaidi.Katika kipindi cha pili tulikuwa bora kwasababu tulianza kucheza kandanda letu katika baadhi ya nyakati.


Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki ijayo jijini London, ambapo Chelsea wanategemwa kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kushambulia na kushinda.


Fußball FC Barcelona Chelsea FC
Lionel Messi kulia akipambana na kiungo wa Chelsea Frank LampardPicha: picture-alliance / dpa

Hata hivyo Hiddink ameonya kuwa Lionel Messi atakuwa mwimba mkali zaidi katika mechi hiyo ya marudiano, akisema kuwa kwa mchezaji kama huyo utaweza tu kumbana usiku mmoja lakini usiku mwengine huwa tofauti.


Messi ndiyo anayeongoza kwa upachika bao katika michuano hiyo ya ligi ya mabingwa akiwaufumania mlango mara nane.


Lakini beki wa Bareclona Gerard Pique alisema kuwa pambano la marudiano litakuwa gumu kwa timu zote mbili.


INSERT:PIQUE


Nadhani litakuwa pambano gumu sana kwa timu zote mbili kwasababu kila timu ni lazima ifunge ili ifuzu kwa fainali na itakuwa vigumu, lakini nafikiri haitakuwa tatizo kwetu kufunga na tutafuzu kwa fainali.


Barcelona katika mechi hiyo ya marudiano itawakosa kiungo wake Yahya Toure na Charles Puyol ambao walionyeshwa kadi za njano.


Kocha wa Barcelona Pep Guardiola alimlaumu refarii wa mechi hiyo au pilato kama washabiki wa kabumbu wanavyopenda kuwaita waamuzi, mjerumani Wolfgang Stark kwa kumuonesha kadi ya njano Puyol kimakosa.


Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman



►◄