1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela akumbukwa

5 Desemba 2014

Wananchi wa Afrika Kusini leo (05.12.2014) wanakumbuka mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi nchini humo baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

https://p.dw.com/p/1DzdC
Mjane wa Mandela, Graca Machel akiwa na shada la mauwa
Mjane wa Mandela, Graca Machel (kushoto) akiwa na shada la mauwaPicha: Reuters/S. Sibeko

Kumbukumbu hiyo imeanza kuadhimishwa kwa misa ya maombi inayojumuisha dini mbalimbali katika jengo la bustani ya Uhuru lililoko mjini Pretoria. Maveterani wa kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo, wamehudhuria ibada ya kuweka mashada ya maua chini ya sanamu ya Mandela, yenye urefu wa mita tano.

Kabla ya kuweka mashada ya maua, mjane wa Mandela, Bibi Graca Machel alisema mwili wa Mandela haupo duniani, lakini roho yake haiwezi kubadilika kamwe na itaendelea kubaikia hivyo daima. Amesema anajua kuwa Mandela anafuraha huko aliko, kwa sababu yeye ni miongoni mwa familia aliyochagua kuijenga.

Aidha, mkuu wa kikabila, Ron Martin amesema miaka ishirini ya demokrasia nchini Afrika Kusini, imewezekana kwa sababu ya Mandela. Kwa upande wake, Ahmed Kathrada, rafiki wa karibu na wa muda mrefu wa Mandela, amesema rais Mandela alikuwa hana makuu na atakumbukwa kwa ubinadamu na ujasiri wake. Wengine walioweka mashada ya maua ni wanafamilia, marafiki wa Mandela, mawaziri, wanawake pamoja na watoto.

Sanamu ya Mandela
Sanamu ya MandelaPicha: Reuters/S. Sibeko

Makamu wa Rais kuongoza dakika tatu za ukimya

Baadaye wananchi wa Afrika Kusini watapuliza vuvuzela, huku honi za magari zikipigwa na kengele zikigongwa kwa dakika tatu na sekunde saba na kufuatiwa na dakika tatu za kukaa kimya, zitakazoongozwa na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Dakika hizo sita na sekunde saba ni kwa ajili ya heshima ya miaka 67 ya utumishi wa umma wa Mandela.

Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa
Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril RamaphosaPicha: DW/A. Lattus

Matukio mengine mengi yamepangwa kufanyika mwishoni mwa juma, ikiwemo kuendesha pikipiki na matamasha. Aidha, mechi ya mchezo wa kriketi itafanyika kama kutoa heshima kwa haiba ya urithi mkubwa aliouacha Mandela, mpinzani mkubwa wa ubaguzi wa rangi na alama ya matumaini duniani.

Wananchi wa Afrika Kusini pia wamekuwa wakitafuta njia mbalimbali za kumkumbuka na kumuenzi Mandela, aliyeiondoa nchi yao kwenye giza. Baadhi yao wamekuwa wakijichora tattoo mwilini, ambapo maeneo maalum ya kuchorea tattoo yamekuwa yakifurika watu.

Tutu awasihi wananchi wa Afrika Kusini

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Mkuu Mstaafu Desmond Tutu, amewataka Waafrika Kusini kuiga mfano wa Mandela wakati wanapoadhimisha kumbukumbu yake. Amesema wajibu wao kwa Mandela ni kuendelea kuijenga jamii ya haki za binaadamu aliyoiacha.

Nelson Mandela alifariki dunia Disemba 5, mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 jela na kazi ngumu, baada ya kuhukumiwa na serikali ya ubaguzi ya Afrika Kusini, kwa kosa la kuendesha shughuli za kupinga ubaguzi wa rangi.

Desmond Tutu ARCHIVBILD 2011
Askofu Mkuu mstaafu Desmonda TutuPicha: picture-alliance/dpa

Baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani mwaka 1990, Mandela alitafuta maridhiano ya kutaka kuwepo Afrika Kusini mpya itakayowafanya watu weusi na weupe kuishi kwa kuzingatia haki sawa. Baada ya utawala wa kibaguzi uliodumu kwa miaka 46 kuanguka, Mandela alishinda urais katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika mwaka 1994 na hivyo kuwa rais wa kwanza mweusi, ambapo alihudumu kwa kipindi cha miaka mitano.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri:Yusuf Saumu