1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manowari za NATO zaelekea bahari ya Aegean

Admin.WagnerD11 Februari 2016

Meli za jumuiya ya kujihami ya NATO ziko njiani kuelekea katika bahari ya Aegean kuzisaidia Uturuki na Ugiriki kuyatokomeza magenge ya wahalifu yenye kuwasafirisha kwa magendo wakimbizi wanaokimbilia barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1HtzW
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg mjini Brussels. (10.02.2016)
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg mjini Brussels. (10.02.2016)Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

"Makao makuu yetu ya kijeshi barani Ulaya SACEUR hivi sasa inaviagiza vikosi vya manowari vya NATO kuelekea Aegean bila ya kuchelewa na kuanza upelelezi wa baharini. Wataalamu wetu wa kijeshi watashughulikia kwa ukamilifu masuala mengine haraka iwezekanavyo na washirika wataangalia njia za kuimarisha shughuli hizo." Katibu Mkuu wa Jumuia ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg akitowa agizo hilo leo hii mjini Brussels katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa jumuiya hiyo.

Stoltenber amesema meli hizo za kivita ambapo hivi sasa ziko chini ya uongozi wa Ujerumani zitafanya upelelezi kusaidia kuumaliza mzozo mbaya kabisa wa wakimbizi kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya tokea kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Meli hizo za kivita zinatarajiwa kuwapatia askari wa mwambao na maafisa wengine wa serikali wa Uturuki na Ugiriki taarifa muhimu.

Shughuli za kikosi

Masaa machache baada ya mawaziri wa ulinzi wa NATO kukubaliana kutumia kikosi chao cha baharini mashariki ya bahari ya Mediterenia kusaidia kupambana na magenge yanayosafirisha watu kwa magendo, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha NATO Generali Philip Breedlove amesema yuko mbioni kushughulikia kwa haraka muundo wa kikosi hicho.

Manowari ya Kijerumani.
Manowari ya Kijerumani.Picha: picture-alliance/dpa/I. Wagner

Ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba wanazipeleka meli hizo kwenye eneo sahihi na kwamba mpango wa kikosi hicho utasanifiwa wakati kikosi hicho kikiwa njiani kuelekea huko ambapo itachukuwa kama saa 24 kufanya hivyo.

Mpango huo ambao mara ya kwanza ulitajwa hapo Jumatatu na Ujerumani na Uturuki umeishtukiza NATO na unakusudia kulisaidia bara la Ulaya kukabiliana na mzozo huo wa wakimbizi ambao ni mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia. Zaidi ya watafuta hifadhi milioni moja wamewasili barani Ulaya mwaka jana.

Breedlove amesema NATO pia itawafuatilia wahalifu hao wanaosafirisha watu kwa magendo katika mpaka wa ardhini kati ya Syria na Uturuki.

Kutokomeza kundi la Dola la Kiislamu

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter pia amezungumzia katika mkutano huo mpango wa nchi yake kupambana na kundi la Dola la Kiislamu.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter mjini Brussels. (11.02. 2016)
Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter mjini Brussels. (11.02. 2016)Picha: Reuters/Y. Herman

Carter amesema "Kampeni ya mpango huo inataka kwanza kabisa na kabla ya yote kutokomezwa kwa kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq kwa sababu hapo ndio mahala inakotoka saratani hii na inatakiwa washindwe huko na miji ya Mosul na Raqaa inatakiwa ikombolewe."

Idadi ya watu wanaokimbnia vita na mataifa yao kushindwa kufanya kazi mashariki ya kati na Afrika Kaskazini haionyeshi dalili ya kupunguwa licha ya hali ya hewa ya kpindi cha baridi ambapo kuvuka bahari inakuwa hatari zaidi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters /AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman