1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaelekea kwenye udikteta

20 Julai 2016

Wasi wasi unazidi nchini Uturuki sambamba na chuki aliyonayo Rais Recep Tayyip Erdogan juu ya wapinzani wake ambao haraka sana baada ya kushindikana jaribio la kuiangusha serikali aliwatangaza kuwa maadui zake.

https://p.dw.com/p/1JSOd
Wafuasi wa Rais Recep Tayyip Erdogan
Wafuasi wa Rais Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Katika maoni yake mwandishi wetu Alexander Kudascheff anasema jaribio la wanajeshi la kumwondoa madarakani limempa Rais Erdogan fursa ya kutimiza lengo moja tu: kuwafagilia mbali wapinzani wake.

Baada ya kushindwa kwa jaribio la kumpindua,Rais Tayyip Erdogan sasa haoni haya wala vibaya .Na kwa sababu ,siyo tu anashambulia kama mbogo anaevuja damu bali pia kwa sababu alikuwa amejitayarisha kwa jaribio hilo. Mashaka yanazidi kuwa makubwa kuhusu mpangilio wa jaribio lenyewe.

Hakuna tena anaezungumzia juu ya ushindi wa umma au wa demokrasia.Sababu ni kwamba jaribio lililofanyika linampa Rais Erdogan fursa ya kulitimiza lengo moja tu: kuwapangusia mbali wapinzani wake.

Guido Westerwell im Interview mit der Deutschen Welle
Picha: DW/M. Hoffmann

Kamata kamata itaendelea nchini Uturuki

Kinachotukia nchini Uturuki ni fagia fagia. Watu zaidi ya 50,000 miongoni mwao,maafisa ,mahakimu na wanasheria wamefukuzwa, au wametiwa ndani.

Kila mtu anaweza kutabiri kwamba watu wengine wengi watatiwa kamba- kutoka tasnia ya habari na kutoka kwenye vyuo vikuu. Uturuki inaelekea dhahiri kwenye utawala wa mtu mmoja kwa kuutumia mwao wa Bunge pamoja na kinachoitwa maslahi ya umma. Rais Erdogan halihitaji Bunge,kwa sababu umma umesimama pamoja naye. Lakini hivyo ndivyo anavyoamini.

Viongozi wa kidini bila shaka wapo katika upande wake. Na hakuna anaeweza kuhakikisha iwapo mfumo wa kutenganisha dini na dola utadumishwa. Hakuna anaeweza kuhakikisha kwamba Uturuki haitageuka kuwa nchi ya kidikteta chini ya Erdogan.

Na mambo yakiwa hivyo,matumaini ya Uturuki kuwemo katika Umoja wa Ulaya yatatoweka, na pia nafasi yake katika mfungamano wa kijeshi wa NATO itakuwamo mashakani. Na mtu akiyasawiri upya yaliyotukia Ijumaa iliyopita ataona kwamba jaribio lililofanywa na wanajeshi lilikuwa kiini macho.

Ndege za jeshi zililishambulia jengo la bunge, lakini hazikuiona sehemu ambako Erdogan alikuwa anafanya mapunziko. Wanajeshi waasi walikitwaa kituo cha radio cha serikali lakini waliviacha vituo vya radio vya watu binafsi. Wala hawakuyakata mawasiliano.

Waliandaa tamthilia yao mapema jioni, mwishoni mwa wiki wakati watu katika mji wa Istanbul wanaburudika ,badala ya kulifanya jaribio wakati ambapo watu wanalala. Pia walimwachia Rais ambae hadi wakati huo alikuwa amoendolewa madarakani apande ndege na arudi katika mji wa Istanbul, kutoka likizoni, ingawa inadaiwa kwamba viongozi wa jeshi la anga walihusika katika njama za kuiangusha serikali. Erdogan aliweza kulakiwa na watu wake.Na askari walifikiri walikuwa wanafanya mazoezi ya kijeshi.

Siyo sahihi kufuata nadharia za uzushi.Lakini jee baada ya miaka mingi ya kuwa Waziri Mkuu na sasa Rais wa nchi hiyo, haitakuwa sahihi kuamini kwamba Erdogan anao watu wake miongoni mwa maafisa wa jeshi?

Kwa nini, asubuhi yake tu baada ya jaribio, Erdogan alikuwanayo orodha ya mahakimu 3000 wa kuwafukuza?

Hata hivyo hakuna ushahidi kwamba Erdogan alilipanga jaribio hilo yeye mwenyewe. Lakini amelitumia jaribio hilo kwa shabaha ya kuwaandama , mahakimu, wale wanaomkosoa, waandishi habari na wote wanaompinga.

Mwandishi:Kudascheff,Alexander

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Josephat Charo