1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bibi Merkel hana haraka juu ya kutoa uamuzi

30 Agosti 2016

Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2013 mambo yalikuwa tofauti kwa Kansela Angela Merkel. Mapema kabla ya uchaguzi huo alitamka wazi kwamba hakuwa anawaza kuondoka kwenye wadhifa huo.Lakini kwa nini amenyamaza?

https://p.dw.com/p/1Jrpv
Kansela wa Ujerumni Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Kansela wa Ujerumani anawaweka Wajerumani katika hali ya tashwishi. Hawajui iwapo Kansela huyo atawania muhula mwingine.Hata hivyo mnamo mwaka wa 2011 mambo yalikuwa shwari kabisa nchini Ujerumani.

Migogoro ya wakati huo ilikuwa mbali na Ujerumani. Ilikuwapo katika nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Umaarufu wa Kansela Merkel miongoni mwa wananchi ulikuwa wa kiwango cha juu kabisa. Kampeni za uchaguzi zilikuwa za upande mmoja na hasa juu yake.

Mgogoro wa wakimbizi wabadilisha hali

Lakini mgogoro wa wakimbizi tangu mwaka uliopita umebadilisha kila kitu.Hisia miongoni mwa wananchi zimegawanyika. Nusu ya wananchi bado wanamwona Merkel kuwa ni kiongozi mzuri. Lakini wengine wanamkosoa, na hata wanafikia hatua ya kuwa na mtazamo mkali juu yake.

Wanachama wengi wa shina kutoka chama chake cha CDU, walikasirishwa kiasi cha kukihama chama hicho na kwenda kujiunga na chama cha mrengo wa kulia cha AfD. Siku ambapo Bibi Merkel alikuwa na umaarufu wa juu kabisa- nyota wa nyota zimepita. Ndiyo sababu kwamba safari hii anapaswa kutegemea uungaji mkono wa chama ndugu cha CSU cha jimbo la Bavaria.

Hatahivyo chama hicho pia kimekasirishwa na sera ya wakimbizi ya Kansela huyo kiasi kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho wametishia kumsimamisha mgombea wao katika uchaguzi. Wengine wametamka wazi kwamba hawatamuunga mkono Angela Merkel.

Maoni wa mwandishi Kay-Alexander Scholz
Maoni wa mwandishi Kay-Alexander Scholz

Mwenyekiti wa chama cha CSU Horst Seehofer anasubiri tu na mpaka sasa anakataa kusema iwapo atamuunga mkono Kansela huyo.

Hali ya kisiasa kwa sasa siyo ya uhakika. Swali muhimu linaloulizwa ni iwapo hali ya usalama itaendelea kuwapo, yaani bila ya kutokea mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani yanayoweza kufanywa na mmoja wa wakimbizi alieruhiswa kuingia nchini Ujerumani.

Mashambulio ya kigaidi yaliyotukia mnamo mwezi wa Julai nchini Ujerumani yameonyesha jinsi umaarufu wa Kansela Merkel na chama chake cha CDU ulivyoanguka vibaya. Chama ndugu cha CSU pia kimo katika hatari ya kuanguka vibaya pamoja na chama cha Kansela Merkel cha CDU.

Katika hali hiyo chama cha CSU kimebakiwa na njia moja tu, yaani kujiweka kando na chama cha Bibi Merkel, cha CDU.

Uchaguzi utafanyika mwezi ujao katika majimbo mawili. Wachunguzi wa maoni wanatabiri ni kwa kiasi gani vyama vya CDU na cha mrengo wa kulia AfD vitakavyojitokeza katika uchaguzi. Pana uwezekeno, huenda chama hicho cha AfD kikaongoza katika jimbo la uzawa la Kansela Merkel Mecklenburg-Western Pomerania. Hayo yatakuwa maafa.

Kwa mujibu wa utabiri mnamo mwaka huu Ujerumani inatarajia kupokea wakimbizi wapya 300,000 tu. Ni idadi ndogo kuliko mwaka uliopita.Lakini utabiti huo unategemea na iwapo mkataba uliofikiwa na Uturuki wa kuwaweka wakimbizi katika nchi hiyo utatekelezwa.

Na ikiwa Ujerumani itaendelea kuwa na usalama hapatakuwapo na kizingiti cha kumzuia bibi Merkel kuwania muhula mwingine.

Chama chake kitafanya mkutano mkuu mnamo mwezi wa Desemba. Na kwa mujibu wa habari za kuaminika mwanasiasa huyo anakusudia kuendelea kuwa Mwenyekiti wa chama chake cha CDU, kwa miaka miwili zaidi.Na kwa ajili hiyo atapaswa, kulijibu swali juu ya kushiriki katika kinyang'anyiro cha kuwania muhula mwingine wa ukansela.

Mwandishi: Scholz, Kay-Alexander .

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga

.