1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kanuni hatari za Putin kwa Ukraine

Klaus Jansen5 Machi 2014

Kwa kutumia nguvu yake ya kijeshi, Urusi inatishia uhuru wa Ukraine siyo tu katika rasi ya Cremea, anasema Johann Bernd. Uingiliaji kati masuala ya ndani ya nchi hiyo ni halali kwa mujibu wa Putin.

https://p.dw.com/p/1BKRi
Deutsche Welle REGIONEN Osteuropa Ukrainisch Bernd Johann
Picha: DW/P. Henriksen

Wakati wasiwasi ukiitawala dunia kwa sababu vita vya rasi ya Cremea vilionekana kama suala la masaa, rais Vladmir Putin alibaki kimya. Sasa rais huyo wa Urusi ameamua kuvunja ukimya wake, akiwaambia waandishi wa habari kuwa Urusi haina nia ya kuiteka Cremea. Lakini ukweli ni kwamba kwa kutumia nguvu yake ya kijeshi katika siku zilizopita, Urusi imekiuka uhuru na mamlaka ya mipaka ya Ukraine si tu katika rasi ya Cremea.

Putin hakuhitaji kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi katika rasi ya Crimea kwa sababu tayari walikuwepo kwa muda mrefu. Maelfu ya wanajeshi wa Urusi wanaohudumu katika meli za kivita zilizo katika bahari nyeusi wamewekwa katika eneo hilo. Zaidi ya hayo walikuja watu wenye silaha wasiokuwa na alama yoyote ya utambulisho kwenye sare zao, na kuzizingira kambi za kijeshi za Ukraine, na pia kuiweka madarakani serikali mpya ambayo ni kibaraka kwa utawala mjini Moscow. Sasa ni zaidi ya kubeza, pale Putin anapojitokeza na kusema kuwa hakuna haja ya kupeleka majeshi huko.

Uingiliaji kati katika mataifa jirani

Uhakika ni kuwa jeshi la Urusi tayari limechukuwa udhibiti wa rasi ya Crimea. Na ukweli ni kwamba katika siku zilizpita, Ukraine ikilipoteza eneo hilo lilioko katika bahari nyeusi. Pengine ni suala tu la wiki chache kabla ya eneo la Crimea kutoka katika mamlaka ya utawala mjini Kiev, baada ya matokeo ya kura ya maoni iliyopangwa kuamua juu ya mustakabali wake.

Lakini kiongozi wa Urusi anataka zaidi. Na ameyabainisha malengo yake kwa uwazi zaidi. Kwamba Urusi inabakiza haki ya kutumia njia zozote zilizopo, ikiwa kutakuwa na machafuko katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine. Pili, Ukraine kulifanyika mapinduzi ya silaha na yanayokiuka katiba. Na tatu uongozi mpya mpya mjini Kiev hauna uhalali wa kuamua juu ya mustakabali wa pamoja wa Ukraine.

Kwa hivyo Putin amebainisha wazi msimamo wake, na unaweza kuingia katika vitabu vya historia kama "Kanuni za Putin." Kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine ni jambo linaloruhusiwa kwa mujibu wa Putin. Kama Urusi haiko tayari kukubali mabadiliko ya serikali katika nchi jirani, basi inaweza kuingilia kati wakati wowote - na ikibidi kwa kutumia nguvu ya kijeshi. Bunge la Urusi llimruhusu Putin kutumia sera kama hiyo, na hii inauweka wazi uwezekano wa kujiingiza kijeshi katika eneo lote la Ukraine.

Ukiukaji wa sheria za kimataifa

Labda Putin atayaacha maeneo ya magharibi na mji mkuu Kiev kwa amani, kwa sababu ni wazi kwamba watu watatoa upinzani mkubwa huko. Lakini katika upande wa wakaazi wengi mashariki, ambako kuna raia wengi wenye asili ya Urusi, Putin anaweza kuthubutu kuingilia kati. Madai ya maombi ya msaada - kama ilivyotokea katika rasi ya Crimea, yanaweza kuwa kisingizio cha kutosha. Hali huko bado haiko bayana baada ya kubadilishwa kwa uongozi mjini Kiev. Uongozi mpya wa Ukraine bado unahangaika kutambuliwa .

Putin anaonyesha yuko tayari kwa mazungumzo baada ya siku kadhaa za ukimya. Lakini Umoja wa Ulaya na Marekani zinapaswa kufahamu wazi kwamba Putin anasisitiza kuwa Ukraine ni sehemu ya mzingo wa ushawishi wa Urusi pasipo kuelegeza msimamo. Kwa hivyo hajali kuvunja sheria za kimataifa, wala makubaliano kati ya Urusi na Ukraine.

Mwandishi: Johann Bernd
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman