1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kuchoma bendera ya Israel si uhuru wa mawazo

Mohammed Khelef
11 Desemba 2017

Licha ya kuwa Ujerumani inaheshimu na kulinda uhuru wa watu kutoa maoni yao kwa namna wapendayo, suala la kuchoma bendera ya Israel halimo kwenye namna hizo na haliwezi kuvumiliwa, anaandika Ines Pohl.

https://p.dw.com/p/2pALi
Deutschland Demonstranten verbrennen Fahne mit Davidstern in Berlin
Picha: picture alliance/dpa/Jüdisches Forum für Demokratie und gegen Antisemitismus e.V.

Haki ya kuandamana inalindwa vyema nchini Ujerumani, isipokuwa tu kwenye mazingira yasiyo ya kawaida ndipo haki hii hubanwa. Kwa hali hiyo hiyo, demokrasia yetu pia imejikuta mara kwa mara ikishuhudia kauli zinazopazwa mitaani hapa Ujerumani  ambazo si za kidemokrasia, kama vile kusema "Wageni waende makwao!"

Nchi yetu imejifunza somo gumu kupitia utawala wa kidikteta wa Manazi, pale ambapo taifa linaweza kwenda endapo dola inaweza kuwanyamazisha wakosoaji wake na kupiga marufuku maandamano mitaani. 

Kwa hivyo, hilo ni suala ambalo wakosoaji wa serikali ya Merkel wanalionesha wanapoandamana au Wapalestina wanapokusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani kuelezea hasira zao dhidi ya mpango wa kuhamishia ubalozi wa Marekani nchini Israel katika mji wa Jerusalem.

Mhariri Mkuu wa DW, Ines Pohl.
Mhariri Mkuu wa DW, Ines Pohl.Picha: DW/P. Böll

Nchi ya wakosaji haipaswi kuangalia kando

Lakini historia yetu haitulazimishi kuruusu kila jambo bila kuweka vikomo. Ni kinyume chake. Ujerumani inabeba dhamana ya mauaji ya Mayahudi takribani milioni sita. 

Na haijalishi kwa muda gani mauaji ya Holocaust yamefanyika, Ujerumani ina jukumu maalum la kupambana dhidi ya chuki kwa Mayahudi. Nchi ya wakosaji haipaswi kamwe kutazama kando. Si popote, na zaidi si katika nchi yako mwenyewe.

Kwa hivyo, kwa namna yoyote ile haiwezakani kukubali bendera yenye nyota ya Daud kuchomwa nchini Ujerumani. Watu wanaotaka hifadhi hapa, wanaotaka kupafanya Ujerumani kuwa nyumbani pao, wanapaswa kuliheshimu hilo. Kuna mambo kwenye jamii yetu ambayo huwezi kuyakiuka.

Ujerumani taifa la wahamiaji

Kwenye jamii nyengine, inaweza kuwa jambo la kawaida kuchoma bendera ili kumdhalilisha adui. Katiba ya Ujerumani imejikita kwenye misingi ya heshima kwa wengine na kuwalinda wachache.

Ingawa hili si sawa na sheria dhidi ya uhalifu, haikubaliki kwa kuzichoma bendera za Uturuki, Urusi, Marekani au Saudi Arabia. Hata kama mtu anaikosoa vikali serikali za nchi mojawapo kati ya hizo.

Kwa Ujerumani kuishi pamoja kama taifa la wahamiaji kunawezekana tu endapo hatusahau kamwe masomo mahsusi kwenye historia yetu mahsusi. Na wale wasioweza kutii hilo, hawana mahala pa kuishi hapa.

Hilo halijadiliki.

Mwandishi: Ines Pohl
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman