1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni kuhusu ziara ya rais Bush Mashariki ya Kati

Maja Dreyer10 Januari 2008

Yaliyozingatiwa hasa na wahariri wa magazeti ya hapa nchini hii leo ni ziara ya rais Bush wa Marekani huko Mashariki ya Kati pamoja na ushindi wa Hillary Clinton katika uchaguzi wa New Hampshire.

https://p.dw.com/p/Cnkq
George W. Bush na Mahmoud Abbas
George W. Bush na Mahmoud AbbasPicha: AP
Kwanza katika udondozi huu ni gazeti la "Volksstimme" la mjini Magdeburg ambalo linasema hivi kuhusu ziara ya rais Bush:
"Rais Bush aliwasili Mashariki ya Kati akiamini kwamba kuna matumaini mazuri amani kupatikana kati ya Waisraeli na Wapalestina. Lakini hakuna watu wengi wenye matumaini haya. Ikiwa Bush anataka kuungwa mkono katika sera zake za Iraq na kudhoofisha Iran itambidi kuzingatia pia maslahi ya Wapalestina. Kwani suala la nchi ya Palestina ndilo chanzo cha mzozo wa Mashariki ya Kati."
Naye mhariri wa "Neue Rheinzeitung" anatathmini hivi nafasi ya rais Bush kuleta amani Mashariki ya Kati:
"Bush hawezi kutoa amri ya kuwepo amani Mashariki ya Kati. Wala hawezi kusaidia chochote kwa sababu haaminiki katika eneo hilo, hususan baada ya vita vya Iraq. Ikiwa kweli anataka ziara yake ifanikiwe lazima atumie urafiki wake na Israel na kuzungumzia wazi sera ya ujenzi wa maskani za wahamiaji wa Kiyahudi kwa vile suala hilo hadi sasa linazuia mazungumzo ya amani."
Tukiendelea na gazeti kubwa la "Bild", mhariri huyu pia haamini kwamba mzozo wa Mashariki ya Kati utaweza kutatuliwa kabla ya rais Bush kumaliza muhula wake madarakani. Hata hivyo, gazeti linasema ziara hiyo si bure.
"Kwa kutembelea eneo hili, Bush anatoa ujumbe ambao unafahamika huko Mashariki ya Kati. Waarabu wanasema: Simba akiondoka, fisi wanacheza ngoma. Maana yake ni kwamba Bush kutembelea mji mkuu wa Israel ni ujumbe kwa wote wanaotumia nguvu na kusababisha fujo. Ujumbe huu ni kwamba mamlaka ya kimataifa ya Marekani yatahakikisha haki ya kuwepo taifa la Israel."
USA Wahlen Demokraten Hillary Rodham Clinton Wahlkampf in New Hampshire
Picha: AP

Naam tuelekee nyumbani kwake Bush ambapo tangu mwanzoni mwa mwaka huu kumefanywa uchaguzi wa wagombea wa urais kwenye ngazi ya chama. Kinachozungumziwa hasa wiki hii ni ushindi wa senata Hillary Clinton jimboni New Hampshire baada ya kushindwa huko Iowa na Barack Obama. Yote hayo ni kinyume na makadirio ya uchunguzi wa maoni. Hili hapa basi ni gazeti la "Neues Deutschland":


"Hillary is back! Ndivyo vyombo vya habari vya Marekani vilivyopiga kelele baada ya ushindi wa Bi Seneta huyu huko New Hampsire. Ni ishara kwamba nchi nzima imeshikwa na homa ya uchaguzi. Ukweli ni kwamba Hillary Clinton hajashindwa. Kinachojulikana hadi sasa ni kwamba uchunguzi wa maoni hazitegemeki."
Na hatimaye tusikie uchambuzi wa mhariri wa "Pforzheimer Zeitung":
"Mara mbili taasisi za kura za maoni zilifanya makosa katika uchunguzi wao. Suali sasa ni je, makadirio yao kwamba Wamarekani wengi wanataka serikali ibadilike na kuchukuliwa na Wademokrats ni kweli?"