1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Majeraha mabichi

Bernd Johann/Mohammed Khelef23 Februari 2015

Huku Ukraine ikiwa inakumbuka mwaka mmoja tangu watu zaidi ya 100 kuuawa kwenye uwanja wa Maidan, lakini Bernd Johann anasema majeraha ya mauaji hayo hayajapona hadi leo.

https://p.dw.com/p/1Efu0
Kumbukumbu za mauaji ya Maidan ambapo zaidi ya watu 100 waliuawa Februari 2014 wakiwa kwenye maandamano mjini Kiev.
Kumbukumbu za mauaji ya Maidan ambapo zaidi ya watu 100 waliuawa Februari 2014 wakiwa kwenye maandamano mjini Kiev.Picha: S. Gallup/Getty Images

Mwezi kama huu mwaka uliopita, raia wa Ukraine waliushinda utawala wa kidikteta na kifisadi. Walichagua demokrasia na mustakabali wa kuelekea Ulaya kwa ajili ya nchi yao. Lakini mwaka mmoja baadaye, mapambano yao kwa ajili ya heshima na uhuru wa kujiamulia yamekumbana na adui mpya na mwenye nguvu zaidi, yaani Urusi.

Kwa kuikhofia Ukraine ya kidemokrasia, Ikulu ya Kremlin imechochea vita barani Ulaya. Serikali ya Urusi inataka kuepuka, kwa gharama yoyote, mustakabali ambao Ukraine inakuwa nchi ya Ulaya, ambapo raia wake wanaweza kuishi kwenye demokrasia, maendeleo na, juu ya yote, kwenye amani.

Kwa miezi kadhaa, maelfu kwa maelfu ya raia wa Ukraine waliandamana dhidi ya mfumo wa kidikteta wa Rais Viktor Yanukovych, wakithubutu kusimama katikati ya baridi kali ya mji wa Kiev na mbele ya ukatili wa dola.

Hatimaye, mabadiliko yakaja, utawala ukaporomoka na watawala wakakimbia Urusi, ambayo hadi hivi leo inaendelea kuyaita maandamano hayo yalikuwa mapinduzi ya kijeshi.

Bernd Johann
Bernd JohannPicha: DW/P. Henriksen

Hayakuwa mapinduzi ya kijeshi

Lakini ukweli ni kuwa mfumo wa utawala uliporomoka kutokea ndani yake wenyewe, maana mwishoni hata vikosi vya usalama vya Yanukovych vilikataa kutii na hivyo kumfanya dikteta huyo mwoga kukimbia.

Hayakuwa mapinduzi, kwani ni baada ya kwamba Yanukovych ameshakimbia kwa muda mrefu, ndipo bunge lilipomtangaza kwamba hana tena madaraka.

Serikali ya Urusi ikajibu hatua hiyo kwa ghasia na ukatili. Ikazikanyagakanyaga sheria za kimataifa kwa kuuchukua mkoa wa Crimea mwezi Machi mwaka jana na kisha kuchochea vita visivyo mwisho mashariki mwa Ukraine.

Hasira dhidi ya serikali ya Ukraine

Baada ya Yanukovych kuondoka, sasa Urusi inataka kuipora haki ya raia wa Ukraine kujiamulia mambo yao wenyewe, bali pia hata heshima yao ya kuwa taifa.

Ndio maana, kwa hayo yote, viongozi wa kimataifa jana waliungana na raia wa Ukraine kuyakumbuka maandamano ya Maidan mwaka mmoja uliopita, pale mlango wa kuelekea kwenye uhuru uliposukumwa na kufunguka.

Mahsusi hasa, raia wa Ukraine wanawakumbuka wenzao zaidi ya 100 waliouawa na wadunguaji wenye silaha. Lakini wanawakumbuka wenzao wakiwa na huzuni, wakiwa na hasira; na hasira hiyo wanaielekezea serikali yao wenyewe.

Sababu ni kwamba hadi hivi leo haijawekwa wazi ni nani aliyeruwarushia risasi waandamanaji na polisi. Nani hasa walioyatenda hayo? Nani hasa aliyewapa amri ya kuivamia Maidan?

Familia za wahanga bado zinangojea majibu. Mfumo wa upatikanaji haki wa Ukraine umeshindwa kwenye uchunguzi wake, na hivyo umeyawacha majeraha yakiwa bado mabichi.

Mwandishi: Bern Johann/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba