1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

maoni mbalimbali baada ya kuachiiwa huru Allan Johnston

4 Julai 2007

Chama cha Hamas kina matarajio kwamba kushiriki kwake katika kuachiliwa mwandishi wa habari wa Uingereza Allan Johnston aliyetekwa nyara mjini Gaza, kutageuza mtazamo wa nchi za magharibi dhidi ya chama hicho.

https://p.dw.com/p/CB34
Allan Johnston Mwandishi wa BBC
Allan Johnston Mwandishi wa BBCPicha: AP

Kiongozi wa chama cha Hamas Ismail Haniya amesema mjini Gaza kwamba anatarajia kuachiliwa kwa mwandishi huyo wa habari wa shirika la BBC siku 114 baada ya kutekwa nyara na koo zenye uwezo mkubwa katika Ukanda wa Gaza kutafungua ukurasa mpya wa mawezekano ya kumuokoa pia mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit aliyetekwa nyara mwaka mmoja uliopita.

Hamas imeelezea kwamba kuachiliwa kwa mateka hao labda huenda kukafungua milango ya kuachiliwa Wapalestina kadhaa wanaozuiliwa katika jela za nchini Israel.

Lakini bibi Miri Eisin msemaji wa waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert ametoa mwito wa kuachiliwa kwa haraka mwanajeshi Gilad Shalit na kulitaja kundi la Hamas kuwa ndio linalohusika na kumteka nyara mwanajeshi huyo.

Hamas, kundi ambalo limetengwa na jamii ya kimataifa kwa muda wa mwaka mmoja, hali hiyo ilidhihirika zaidi pale vikosi vya chama hicho vilipowazidi nguvu wanajeshi watiifu kwa kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas hapo Juni 15 walipoliteka eneo la Ukanda wa Gaza.

Vikosi hivyo hivyo ndio leo vimeonekana mbele ya kamera za wanahabari wa kimatiafa vilipompeleka mwandishi wa habari wa BBC Allan Johnston mbele ya maafisa wakuu wa chama cha Hamas.

Ismail Haniya aliyekuwa waziri mkuu wa Palestina ambae alifutwa kazi na rais Mahmoud Abbas amesema kwamba hatua iliyotimizwa na chama chake ni dhihirisho tosha kuwa kuna usalama na utulivu katika Ukanda wa Gaza.

Allan Johnston mwenye umri wa miaka 45 ametoa shukurani zake kwa chama hicho cha Hamas kwa juhudi kilizofanya mpaka kuachiliwa kwake huru.

Lakini chama cha Fatah chenye mtazamo wa kadiri kimelilaumu kundi la Hamas kwa utekaji nyara wa mwandishi huyo wa habari wa BBC.

Mchambuzi wa taasisi ya kimataifa inayoshughulikia migogoro duniani, Moin Rabbani amesema kwamba kuachiliwa kwa Allan Johnston ni ushindi mkubwa kwa chama cha Hamas katika jitihada za kuimarisha usalama na wakati huo huo ni ujumbe kwa nchi za magharibi zinazolipinga kundi hilo na kumpendelea rais Mahmoud Abbas.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Miliband ametambua mchango mkubwa uliotolewa na Ismail Haniya juu ya kuachiliwa Allan Johnston.

Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na Ismail Haniya kwa pamoja walilaani vikali kutekwa nyara mwandishi habari Allan Johnston na wote walitoa mwito wa kauchiliwa kwake huru haraka iwezekanavyo.