1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Huo haukuwa mdahalo

Iddi Ssessanga
4 Septemba 2017

Kufuatia mdahalo wa pekee wa uchaguzi kati ya Angela Merkel na Martin Schulz, jambo moja limedhihirika - kutohitajika kwa serikali nyengine ya muungano kati ya vyama vikuuu viwili! Anasema mhariri wa DW Christoph Strack.

https://p.dw.com/p/2jLDt
Bundestagswahl TV-Duell Merkel skeptisch Schulz ernst
Picha: Reuters/RTL

Hilo halikuwa shindano. Na wala huwezi kusema kwamba lilikuwa pambano. Kile kilichotajwa kuwa mdahalo wa Televisheni na kuonyeshwa kwenye vituo vikuu vitano vya televisheni vya Ujerumani, yumkini ndiyo ulikuwa mdahalo dhaifu zaidi tangu mfumo huo ulipoanzishwa mwaka 2002. Na ulieleza mengi kuhusu siasa za Ujerumani kama ulivyofanya kuhusu televisheni nchini humo.

Pamoja, siyo dhidi

Kansela Merkel alisimama dhidi ya, au sambamba na mpinzani wake Msocial Democratic, Martin Schulz. Ulikuwa mdahalo uliowahusisha wanasiasa wawili - ambao vyama vyao vimekuwa vikiitawala Ujerumani kwa pamoja katika serikali ya muungano kwa miaka minne iliopita - dhidi ya waandishi wanne wa habari, huku umma ukilaazimika kusalia kimya na kuangalia tu.

Christoph Strack
Mhariri wa DW Berlin, Christoph StrackPicha: KNA

Licha ya uchumi imara wa Ujerumani, ugumu wa kijamii unaweza kuwepo. Hata hivyo, kwa kuangalia mdahalo wa Jumapili, ungeweza kudhani hali sivyo ilivyo, kwa sababu suala hilo lilitajwa kwa nadra katika muda wote wa dakika 97 za mdahalo huo. Ugumu unaozikabili familia nyingi, changamoto na fursa za mfumo wa digitali na teknolojia, na utandawazi wa nafasi za ajira na elimu - masuala yote ambayo hayakupata furusa ya kuzungumziwa.

Badala yake, ilikuwa kana kwamba tumerejeshwa nyuma katika mwaka wa 2015, huku mdahalo ukijikita zaidi juu ya upokeaji na utangamano wa wakimbizi. Bila shaka wanasiasa wanapaswa pia kukabiliana na hasira zilizozidi kujidhihirisha katika kipindi cha miaka miwili iliopita, katika miji na vile vile maeneo ya vijijini. Lakini kwa mara nyingine siasa kali za kizalendo zimedhoofisha juhudi na uweledi wa kazi ya siasa.

Kulikuwepo na masuala kadhaa ya sera ya kigeni hata hivyo. Kuhusu Uturuki, wagombea wote walitangaza mabadiliko ya kijasiri katika mwelekeo: Hakuna majadiliano tena juu ya kupanua umoja wa forodha na hakuna tena mjadiliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya. Chama cha SPD kilitaka kuacha wazi suala la uanachama wa Umoja wa Ulaya, huku vyama vya kihafidhina vimekuwa vikitaka kuzuwia kabisaa jambo hilo. Na mnamo wakati kuna mtawala wa chuma mjini Ankara, ambaye anaichukulia mateka Ujerumani, sera ya Ujerumani kuhusu Uturuki inaanza kubadilika pakubwa.

Jambo la pili, kuhusu mgogoro wa Korea Kaskazini, Merkel aliweza kutumia uzowefu wake wa kiongozi wa serikali na kuorodhesha simu zake zijazo na viongozi mijini Moscow, Beijing, Tokyo, Seoul na Washington. Tatu, Merkel na Schulz wote walikubaliana kwamba Qatar haikuwa mwenyeji anaestahiki wa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2022. Ni nadra kusikia mwanasiasa, na isitoshe wawili, wakilizungumzia hilo kwa uwazi namna hiyo. Tulizingatie hilo mara nyingine tukiwaona viongozi wa kitaifa wakisafiri kwenda taifa hilo la Ghuba na ujumbe wao wa wawakilishi wa biashara.

Deutschland TV Duell Merkel - Schulz
Merkel na Schulz wakiwa katika mdahalo wa televisheni Jumapili jioni, 03.09.2017.Picha: Reuters/F. Bensch

Kutoweka taratibu

Iwapo dakika 97 za mdahalo zilikuwa na kitu cha kuonyesha, basi kilikuwa kwamba Ujerumani haihitaji tena serikali ya muungano mkuu. Tafadhali, hapana tena. Vyama hivyo viwili vimedhibiti bunge la shirikisho Bundestag kwa muda mrefu kupita kiasi. Mbali na hilo, ilikuwa dhahiri Jumapili jioni kwamba hawawezi kuvumiliana tena. Wanajua kila ufa uliopo katika ukuta wa kila mmoja wao.

Demokrasia inahitaji serikali imara, lakini inahitaji pia upinzani imara. Mdahalo na upinzani dunia unaondoa hilo. Tangu 2005, mdahalo wa televisheni umeendelea kuwa jambo la mara moja katika kila uchaguzi wa shirikisho. Ni bora namna hii. Mfumo wa Ujerumani ni wa demokrasia ya kibunge na siyo wa urais.

Mfumo wa Ujerumani unajikita juu ya chaguo la vyama, na siyo kiongozi wa serikali. Demokrasia ya mfumo wa bunge inahitaji sera imara na sauti ya upinzani. Siku ya Jumapili jioni, tuliona masuala haya yote yakijotokeza usoni, wakati mailioni ya Wajerumani wakiangalia mdahalo huo.

Mwandishi: Christoph Strack/DW Berlin

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman