1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Muhula wa nne wa Merkel ni mgumu kwake

Mohammed Khelef
14 Machi 2018

Licha ya Kansela Angela Merkel kufanikiwa kuchaguliwa tena kuongoza serikali ya shirikisho la Ujerumani kwa muhula wake wa nne madarakani, Christoph Strack wa DW anasema kiongozi huyu mkongwe ana wakati mgumu zaidi.

https://p.dw.com/p/2uK0Y
Deutschland Vereidigung der Bundeskanzlerin
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Matokeo yanatosha. Angela Merkel ndiye kansela kwa mara nyengine. Kwa mara ya nne, bunge la Ujerumani limemchaguwa mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 63, ingawa lwa uchache wajumbe 35 wa bunge wa shirikisho wamemkatalia, na matokeo yake amepata kura 9 tu za ziada ya zile ambazo alikuwa anahitajika.

Ushindi huu ufinyu umekuwa ni kawaida kwa serikali za mseto za muungano uitwao mkuu, ambapo vyama ndugu vya kihafidhina, CDU/CSU, hupaswa kushirikiana na Social Democrat kwa sababu maalum. 

Katika mwaka 2005 na 2013, asilimia baina ya nane hadi kumi ya kura za vyama vinavyounda serikali ya mseto zilikosekana kwenye kura ya siri. Lakini wingi wa kura za kansela ni wingi wa kura za kansela tu. Daima hutosha, wala hakuna jengine.

Baada ya miezi sita ya kuwako kwenye mkwamo, uchaguzi huu wa leo ni ishara. Baada ya mkwamo huo, muungano mkuu umetangaza neno “mpya” kuwa moya ya dhana muhimu za makubaliano ya serikali yao ya mseto. Kama mtu alikuwa anatazamia ishara nyengine ya kuashiria umoja ndani yao, haipo. Hata hivyo, hii nayo ni ishara.

Changamoto kwa Merkel na washirika wake

DW Intranet Christoph Strack
Christoph StrackPicha: DW

Licha ya yote hayo, la muhimu ni kuwa sasa Ujerumani ina kansela anayetawala, ina serikali kuu ya shirikisho inayofanya kazi zake. Hicho ni kitu chema kwa sababu kukosekana kwake kulikuwa kunaleta changamoto kubwa za ndani na nje.

Mdahalo mkali juu ya kazi za shirika la hiari la Tafel na umasikini unaonesha mwamko mpya kwenye jamii ya Kijerumani, ambayo kwa muda mrefu haikuwa imekabiliwa moja kwa moja na suala la wakimbizi.

Kimataifa, Ulaya nzima na hasa Rais Emmanuel Macron, walikuwa wakingojea kwa hamu na ghamu serikali hii. Pamoja hayo, kuna mengine kadhaa yanayoihitaji Ujerumani imara kama vile kitisho cha vita vya kibiashara na Marekani, staili ya utawala wa Donald Trump, mtafaruku kati ya Uingereza na Urusi, kwa kutaja changamoto chache za kimataifa. 

Kwa vyovyote, kuchaguliwa leo kwa kansela ni mwisho wa siku 171 za mapambano ya kisiasa, safari iliyoanza kwenye uwezekano wa kuwa na serikali ya mseto wa Jamaica, kisha ikaingia kipindi cha mpasuko wa kisiasa hadi kwenye kuvunjika moyo na hatimaye kwenye kile kinachoonekana kuwa ni safari mpya lakini kongwe.

Kitu kimoja kilicho wazi ni kwamba siku hizo 171 zilionesha kuwa mfumo wa kisiasa wa Ujerumani umejitayarisha kwa changamoto kama hizi. Hilo ni ishara nzuri. Lakini Wajerumani wanapaswa kuwa na umakini zaidi katika kutathamini michakato ya kisiasa kwenye mataifa mengine yaliyopaswa kukabiliana na vigingi kama hivi katika nyakati ngumu kiuchumi.

Kwa Merkel, muhula wake wa nne kwake mpya tena, yumkini hata ukawa ndio wenye majaribu makubwa pia. 

Mwandishi: Christoph Strack/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga