1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ni vyema Croatia kuingia Umoja wa Ulaya

Christina Ruta1 Julai 2013

Croatia inajiunga rasmi na Umoja wa Ulaya katika wakati ambapo Umoja wenyewe uikabiliwa na mgogoro wa sarafu ya euro na wakosoaji wanahofia kuwa nchi hiyo itakuwa dimbwi jengine la machafuko ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/18yud

Mwaka 2004, pale mataifa kumi yalipojiunga na Umoja wa Ulaya kwa mkupuo mmoja, tuliandika kwamba hilo hapana shaka lilikuwa tukio la kupongezwa na la aina yake.

Lakini leo, ambapo kuna mashaka ndani ya eneo linalotumia sarafu ya euro kwenye Umoja huo, hata gazeti la Bild la Ujerumani limeandika “Croatia Kaburi jengine la mabilioni”, kwa maana ya kusema nayo itakuja kulazimika kupatiwa mabilioni ya euro ya kuuokoa uchumi wake.

Na Verica Spasovska
Na Verica SpasovskaPicha: DW/P. Henriksen

Wengine wanaichukulia kama nchi iliyojaa ufisadi na ambayo inakabiliwa na siasa kali za kihafidhina, hasa panapohusika na mahusiano yake na Serbia.

Wanasiasa wa Croatia wanajuwa vyema kwamba licha ya kuondoka kwa ile hofu ya mwanzo iliyofanya ichukuwe muda mrefu kwa nchi yao kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, bado kupewa wenyewe tu uwanachama hakufanyi mambo yote yawe safi kufumba na kufumbua.

Ni nchi iliyojitahidi

Bado kuna mengi ambayo wanasiasa wa Zagreb wanapaswa kuyafanya ili hasa kuwa mwanachama mwenye sifa na heshima zote. Na miongoni mwa hayo ni pamoja na mageuzi ya kimsingi kwenye mfumo wa uchumi, utawala, na mapambano dhidi ya ufisadi.

Hata hivyo, shaka hizi haziondoshi ukweli mwengine mmoja: kwamba kwa miaka kadhaa sasa Croatia imekuwa ikipiga hatua mbele kwenye takribani maeneo yote. Ndiyo maana, hata timu ya tathmini ya Umoja wa Ulaya juu ya suala la ufisadi, ilisema kwamba Croatia iko kwenye nafasi bora zaidi ikilinganishwa na mataifa kama Bulgaria na Romalia, ambayo tayari ni wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Jambo jengine lililoipa sifa nchi hiyo iliyotokea kwenye vita si zaidi ya miaka 20 sasa, ni kushirikiana kwake na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita juu ya iliyokuwa Yugoslavia, mjini The Hague.

Uichukuwapo ukaiweka kwenye mizani hivi leo, Croatia sio tena ile ya mara tu baada ya vita: ya leo una kiwango fulani cha uvumilivu na uwazi na imepiga hatua kubwa kuelekea utawala unaozingatia sheria.

Na wala haiwezi kukanushwa kwamba yote hayo yasingeliwezekana kama hapakuwa na kichochea cha maombi ya uwanachama kwenye Umoja wa Ulaya.

Kwa maana nyengine, mtu anaweza kusema kwamba Umoja huo umeisaidia Croatia kuweka sawa nyumba yake, kabla haijaomba na kukubaliwa mahusiano na wengine, mahusiano ambayo yanamaanisha kuchangiana na kubebana kwa mengi, ya pawa na miko.

Jambo moja lapaswa kufahamika na wale wakosoaji, kwamba kujiunga na Umoja wa Ulaya hakukaribishi tu mizigo, bali marafiki na washirika kwenye Umoja huo, ambao mchango wao unahitajika. Hasa kwa nchi kama Ujerumani, ambayo kutanuka kwa Umoja wa Ulaya kunamaanisha kutanuka kwa soko la bidhaa zake na la ajira pia.

Bila ya kusahau nukta nyengine muhimu, kama tunauchukulia Umoja wa Ulaya kwenye kipimo cha faida na hasara tu: ikumbukwe kwamba Umoja wenyewe ulikuwa na unaendelea kuwa mradi wa kuleta amani ulioanzishwa baada ya madhara makubwa ya Vita vya Pili vya Dunia.

Mkakati wa kuutanua Umoja huu na kuyashirikisha mataifa ya Balkan ya Magharibi ni nyenzo ya kuhakikisha usalama kwenye eneo hilo, ambalo kwa vyovyote ni Ulaya tu! Wakroatia wanaishi kwenye taifa ambalo bado lina kumbukumbu mbichi za vita. Na katika mazingira kama hayo, hakuna asiyejua namna amani ilivyo mtegoni. Uzoefu huu unaweza kutumika kuliimarisha wazo la Ulaya moja.

Mwandishi: Verica Spasovska
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo