1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ugaidi ni hofu

23 Julai 2016

Hofu na taharuki mjini Munich. Shambulizi la umwagaji damu katika eneo la maduka la Olympia katika mji mkuu huo wa jimbo la Bavaria limeitikisa mno Ujerumani mpaka katika misingi yake.

https://p.dw.com/p/1JUk4
Deutschland Olympia Einkaufszentrum in München Hauptbahnhof Polizei
Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Ujerumani iko katika mshutuko kufuatia mashambulizi ya mjini Munich na sasa inakabiliwa na changamoto kubwa, anasema mwandishi wetu, Christoph Strack, katika maoni yake.

Umekuwa usiku mbaya sana na wenye majonzi. Risasi zilifyatuliwa, watu wengi walijeruhiwa na kiasi watu kumi wameuawa. Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu ugaidi, ingawa mpaka sasa hakujawa na thibitisho.

Lakini kwa walioshuhudia shambulizi la mjini Munich, bila shaka lilikuwa la kigaidi. Na shambulio hili kutokea katika mji mkuu wenye fahari wa jimbo la Bavaria, jimbo linalojulikana sana kwa ulinzi kabambe wa polisi, na ambao pia umekosolewa kwa sera zake hizo.

Ugaidi ni hofu. Na hofu imewasili Ujerumani, katika miji yake mikubwa. Hofu iliyoikumba Norway miaka mitano iliyopita, wakati Behring Breivik alipofanya mauaji ya kiholela mjini Oslo na katika kisiwa cha Utoya. Na hofu ambayo wiki moja tu ilishuhudiwa katika barabara za mji wa Nice nchini Ufaransa, wakati maisha ya watu 84 yalipokatizwa ghafla kinyama wakati waliposherehekea sikukuu ya taifa ya Bastille.

Chuki inatoka wapi?

Siku chache baadaye, mkimbizi kijana kutoka Afghanistan aliwajeruhiwa watalii kadhaa kutoka China katika mashambulizi ya shoka na kisu ndani treni karibu na mji wa Würzburg, pia katika jimbo la Bavaria.

Kwa mara ya kwanza Ujerumani imekutana uso kwa uso na chuki, kutoka kwa mkimbizi wa umri wa miaka 17 aliyewashambulia watu na nchi ambayo ilijitolea kwa dhati kumsaidia.

Strack Christoph Kommentarbild App
Mwandishi wa DW, Christoph StrackPicha: DW

Baada ya mashambulizi ya Ijumaa mjini Munich, hata hivyo, kitu kimoja ni bayana: Sababu na misingi wa tukio hili la kusitisha inabaki kuwa kitendawili ambacho hakichateguliwa. Shutuma za haraka lazima ziepukwe.

Lakini pamoja na hayo, maswali mengi yangalipo. Maswali haya yanahitaji majibu - ingawa majibu haya huenda yasipatikane, na lolote litakalopatikana yumkini likasababisha uchungu mkubwa. Kwa sasa, lazima tumshukuru kila afisa wa polisi anayetulinda - wakati mwingine hata katika mazingira ya kuhatarisha maisha yao wenyewe.

Mitandao ya kijamii

Na kuna kile kinachoitwa mitandao ya kijamii, ambayo wakati kama huu hutumika sana kusambaza taarifa. Dakika chache baada ya vifo vya kwanza kuthibitishwa, wakati watu walipokuwa wakiishi katika hofu, maoni ya kwanza yalijitokeza katika mtandao wa kijamii wa Twitter yakishangilia uwezekano wa kujiuzulu au kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Pia hili: Vituo vya televisheni vilijaa picha za video kutoka eneo la maduka la Olypmia, picha zilizojaa mtafaruku. Picha hizi zilielezwa kuonyeshwa moja kwa moja - lakini wakati huo huo, wakaazi wa Munich walikuwa wakihofia maisha yao. Hata vyombo vya habari vinapaswa kujifunza kujizuia nyakati kama hizi.

Hakikisho la kimya kimya kwamba ugaidi ulitokea tu katika mataifa ya nje - Ufaransa, Ubelgiji, Tunisia, Marekani, Uingereza na Uturuki, miongoni mwa mengine, sasa limeyeyuka na halipo tena. Na mtu hapaswi kusahau kwamba mjini Istanbul nchini Uturuki au Nice, Ufaransa, Wajerumani pia waliuawa.

Chochote kitakachotokea katika siku zijazo, Ujerumani bila shaka itakuwa nchi iliyobadilika. Nchi inakabiliwa na mtihani - mtihani ambao utayapa changamoto maingiliano ya kijamii Ujerumani, ari yake, mamlaka zake na uwezo wa serikali katika masuala ya uongozi. Lakini pia itahitaji uaminifu linapokuja suala la kuyashughulikia matatizo yanayoongezeka - iwe ni ugaidi wa makundi ya kiislamu au chuki ya jamii iliyogawika.

Mwandishi:Strack, Christoph

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Isaac Gamba