1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Tahadhari si udhaifu

Sabine Kinkartz/Mohammed Khelef18 Novemba 2015

Ingawa magaidi wangelipenda kuwaona watu wanaowatisha wakitishika na kujifungia majumbani mwao kwa wasiwasi na hofu, Sabine Kinkartz anasema kuchukuwa tahadhari si jambo la kuonesha udhaifu.

https://p.dw.com/p/1H7bJ
Frankreich Schießerei bei Polizeiaktion in Saint-Denis Paris
Picha: Reuters/J. Naegelen

Kama kuna kitu ambacho magaidi wangelikitaka hapa barani Ulaya ni kupandikiza khofu na wasiwasi miongoni mwa raia na serikali zao na kuyafanya maisha yawe ya kutokujiamini na hivyo ile dhana ya uhuru, utulivu na demokrasia inayoheshimiwa kama misingi ya jamii za Ulaya iwe haina maana yoyote kwenye maisha ya watu.

Mechi ya kirafiki ya mpira iliyokusudiwa kuonesha mshikamanao na uhuru kati ya Ujerumani na Uholanzi imeahirishwa mjini Hannover dakika 90 kabla ya mchezo kuanza. Hofu kwamba kungelikuwa na mashambulizi ya kigaidi. Ndege mbili za Shirika la Ndege la Ufaransa, moja kutoka Los Angeles, Marekani, kwenda Paris, Ufaransa, na nyengine kutoka Washington kwenda pwani ya mashariki ya Canada, zimelazimika kutua maeneo tafauti kwa ukaguzi. Nazo kutokana na hofu ya kuripuliwa na magaidi.

Hiki ni kidonge kichungu mno kukimeza lakini ndicho kinachotueleza ukweli wenyewe na kutufanya tujiulize maswali: Hivi magaidi tayari wameshashinda? Je, wamefanikiwa kupandikiza khofu kiasi hicho kwamba tayari tunatetemeka? Je, tupo kwenye mtafaruku kiasi hicho kwamba mechi ambayo ilikuwa imepangwa kuwa alama kubwa ya uthubutu wa watu wa Ulaya ilipaswa kufutwa dakika za mwisho? Kwamba watu wote, akiwemo Kansela na mawaziri wake, ambao walipaswa kuingia uwanjani hapo kifua juu kwa fahari, wanapaswa kurejea nyuma kulinda usalama wao?

Sabine Kinkartz
Sabine KinkartzPicha: DW/S. Eichberg

Tahadhari si udhaifu

Ni hisia chungu za kugugumia ndani kwa ndani ambazo zinakuwa sasa. Na sio tu kwamba mashabiki wengi wa soka wanaohoji ikiwa kufuta mchezo huo lilikuwa kweli jambo la lazima. Waziri wa Mambo ya Ndani, Thomas de Maiziere, anaamini kwamba lilikuwa, lakini bado anapaswa kutoa maelezo zaidi ya kuushawishi umma.

Badala yake, anautaka umma umpe husnu-dhanna - umfikirie kuwa alikuwa na nia njema. Hataki kueleza yasiyo na uhakika lakini wakati huo huo hataki kuingilia upelelezi. Na hilo lingelitokezea lau mambo mengi yangelifichuliwa katikati ya uchunguzi unaoendelea.

Kwa juu juu, kulikuwa na sababu nzuri ya kuifuta mechi hiyo. Ushahidi wa kuwepo mipango ya mashambulizi iliyoripotiwa ulikuwa unashawishi mno kufikia mapema jioni ya jana kiasi cha kwamba ufutaji wa mchezo huo ulikuwa hauepukiki. Lakini ikiwa mimi nashawishika na hatua hii, wengine watakuwa wanasema: "Hapana shaka, waziri na timu yake ya usalama wamechukuwa hatua kubwa zaidi kwa uvumi tu au upotoshaji." Wengine watawaona kabisa kuwa wamefanya makosa.

Kama ilivyotokea mjini Aachen, ambako kufuatia taarifa za kupewa tu, polisi waliwakamata watu saba na ikasemwa kwamba tayari pamepatikana pa kuanzia kwenye upelelezi wa mashambulizi ya Paris, lakini masaa kumi baadaye wote wakaachiwa huru kwa kuwa hawakuwa wakihusika na chochote kile.

Kuthubutu kila siku ni jambo jema, lakini panapokuwa na mashaka lazima tahadhari ichukuliwe, kama ilivyokuwa jioni ya jana ambapo baada ya kuwepo kwa mashaka makubwa, mechi ya Hannover ikafutwa. Au kama ilivyokuwa kwa ndege za shirika la ndege la Ufaransa kupelekwa kwengine kwanza kuhakikisha kuwa ziko salama.

Mwandishi: Sabine Kinkartz
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba