1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dini: Uhuru ni haki ya binaadamu

Felix Steiner15 Januari 2015

Wakati papa Francis amehitimisha ziara yake nchini Sri Lanka, ujumbe mkuu wa kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani ni wa kuzingatiwa na ulimwengu mzima, anasema mwandishi wa DW Petersmann Sandra.

https://p.dw.com/p/1EKkY
Papst Franziskus Messe in Colombo 14.01.2015
Picha: Reuters/D. Liyanawatte

Dini kamwe haiwezi kuwa kisingizio cha kufanya vurugu. Na maridhiano hayawezekani bila ukweli kubainishwa. Masuala hayo mawili ndiyo yalibeba ujumbe mkuu wa ziara ya papa nchini Sri Lanka. Mtu hapaswi kuipenda Vatikan au kuwa Mkatoliki safi ili kuona umuhimu wa ujumbe huu. Ndiyo maneno sahihi kwa wakati sahihi.

Sri Lanka ndiyo imekamilisha mchakato wa mabadiliko ya uongozi ambao haukuwa unatarajiwa. Taifa hilo la kisiwa lenye wakaazi karibu milioni 21 halionekani mara kwa mara kwenye jukwaa la habari za kimataifa - ambalo pia lilitokana na ukweli kwamba serikali iliyoondolewa ya rais Mahinda Rajapaksa ilikuwa imeukanyaga uhuru wa vyombo vya habari. Wakati huo huo lulu hiyo ya bahari ya Hindi imezidi kupendwa na watalii, hata kutoka Ujerumani. Kisicho bayana ni iwapo wasafiri wanaipenda pia nchi hiyo na watu wake.

Mwandishi wa DW Petersmann Sandra.
Mwandishi wa DW Petersmann Sandra.

Ziara katika taifa lililogawika

Papa amefanya ziara katika wakati nyeti kisiasa, kwenye taifa lililoko pembezoni. Taifa dogo ambako matatizo mengi ya ulimwengu mpana wa sasa yanaakisiwa. Sri Lanka ni nchi yenye makabila mengi, dini nyingi na imegawika. Nchi hiyo ndiyo inaanza kutibu majeraha ya vita vya ugaidi vilivyodumu kwa karibu miongo mitatu.

Mwaka 2009 jeshi lililisambaratisha kundi la waasi wa kabila la Tamil, ambalo lilikuwa likiwatumia watoto na waripuaji wa kujiota muhanga kulaazimisha kuunda taifa huru la Watamil. Katika vita vya mwisho vilivyopiganwa kwenye ukanda mdogo wa pwani ya kaskazini, waasi wa Tamil waliwatumia raia kama ngao - wakati jeshi lililokuwa linasonga mbele, liliuwa na kushinda.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, pande zote mbili zilihusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Hata hivyo, baada ya ushindi serikali ilikwenda na kuchora msitari na Sri Lanka ya kaskazini ya Watamil iliendelea kuwa ukanda maalumu wa vita. Hakukuwa na juhudi zozote za maridhiano wala upatanishi hadi hii leo. Watu kutoka kabila la walio wengi la Sinhale wanahodhi nafasi zote muhimu katika serikali, jeshi na uongozi.

Dini yao ya Budha, inaonyesha kuwa dini yoyote inaweza kuwa na sura ya chuki na itikadi kali - kila wakati watu wanapotumia dini kama silaha dhidi ya watu wengine. Sri Lanka imeshuhudia katika miaka iliyopita, mamia ya mashambulizi dhidi ya Wahindu wa kabila ya Tamil, na pia dhidi ya makundi ya dini za wachache - Wakristu na Waislamu.

Nafasi ya maridhiano

Baada ya utawala wa miaka kumi wa Rajapaksa, Sri Lanka sasa ina rais mpya. Mbudha Maithripala Sirisena alishukuru ushindi wake hasa kwa wapiga kura wa Tamil, na Waislamu na Wakristu wa Sri Lanka. Sirisena sasa anaweza kujenga demokrasia imara nchini Sri Lanka, ikiwa atazingatia ujumbe wa kimataifa wa papa, unaosema: Kamwe dini isitumiwe kwa kisingizio cha vurugu. Na maridhiano bila ukweli hayawezekani.

Mwandishi: Petersmann Sandra.
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba