1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wa ndani Ujerumani, mjadala uko wazi

5 Januari 2017

Kutokea kwa shambulizi kubwa la kigaidi, na kukaribia kwa uchaguzi mkuu, ni masuala mawili yanayowafanya wajerumani kwa wakati huu kujadili njia bora za usalama wa nchi yao. Fabian von der Mark wa DW anasema wanayo haki.

https://p.dw.com/p/2VJSG

Mnamo siku ya kwanza ya kazi ya mwaka 2017, mkuu wa chama cha Social Democrats, SPD alitangaza fikra zake kuhusu usalama wa taifa. Siku ya pili, waziri wa mambo ya ndani kutoka chama cha Christian Democratic Union, CDU akafanya hivyo hivyo, na siku ya tatu, ilikuwa zamu ya chama ndugu na CDU, yaani Christian Social Union, CSU. Vyama vingine muhimu, vikiwemo kile cha walinzi wa mazingira, chama cha mrengo wa Kushoto-Die Linke, Free Democrats, FDP na kile cha mrengo mkali wa kizalendo cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD vile vile vimeufanya usalama wa ndani kuwa suala la kipaumbele.

von der Mark Fabian Kommentarbild App
Fabian von der Mark, DW

Inaweza kusikika kama harakati za kisiasa ambazo ni za kawaida baada ya kufanyika shambulizi. Lakini, kwa hali halisi, vyama vya kisiasa vya Ujerumani vimo katika mashindano ya kupata dhana bora ya usalama wa taifa. Hili ni suala ambalo linazigusa nyoyo za raia. Hofu na sintofahamu vimeongezeka, na kila mtu anasubiri kuona majibu yatakayotolewa na wanasiasa.

Swali kubwa linalojadiliwa ni kuhusu kamera katika maeneo ya umma. Baada ya shambulizi kwenye soko la Krismasi mjini Berlin, watu wanauliza kwa nini hakuna picha za mshambuliaji, Anis Amri akikimbia kutoka eneo la tukio. Jibu, ni kwa sababu nchini Ujerumani maeneo ya umma hayachunguzwi sana, kwa sababu siku za nyuma, watu walihofu kuchunguzwa na serikali, kuliko uhalifu. Lakini kwa wakati huu ambapo vyama vya SPD na CDU vikiunga mkono kuwepo kwa kamera zaidi, na vyama vingine, hususan FDP vikipinga, litakuwa jukumu la wananchi kufanya maamuzi.

Bangili kwenye kifundo cha washukiwa?

Swali jingine ni juu ya namna ya kuwashughulikia wale ambao wako katika orodha ya serikali, wakishukiwa kuweza kufanya shambulizi la kigaidi, kama Anis Amri. Serikali inasema watu 550 wako kwenye orodha hiyo, baadhi nyendo zao zikichunguzwa kwa karibu, wengine wakiachwa tu. Je, ingekuwa sawa kuwashitaki watu kwa kutoa kauli zinazounga mkono itikadi kali za kiislamu? Je watu hao wanapaswa kuvishwa bangili maalumu ili wajulikane mahali walipo, au ni bora tu kuviongezea maafisa vikosi vya polisi kama inavyopendelewa na chama cha SPD?

Maswali yote kuhusu usalama wa taifa hayalingani katika kuhamasisha hisia, wala kwa umuhimu, au kwa utata wake. Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere anataka polisi ya shirikisho ipewe nguvu zaidi kuweza kukabiliana na ugaidi katika nchi nzima. Kwa sasa, idara 17 za polisi nchini Ujerumani zinalazimika kubadilishana taarifa kuhusu kesi ya mtu kama Anis Amri, ambaye amesafiri kupitia ujerumani na Ulaya. Je isingekuwa bora kuwa na idara moja ya polisi ya Ujerumani nzima, inayowasiliana na idara nyingine za Ulaya. Majukumu ya polisi na idara za upelelezi kwa ngazi ya jimbo yanashughulikiwa na serikali za majimbo. Chama cha CSU cha Bavaria, kinatarajiwa kuchukuwa msimamo mkali kuhusu pendekezo la kuyahamishia majukumu hayo katika serikali kuu.

Haja ya kurahisisha mambo

Na kuna suali juu ya nini kifanywe kuhusu watu ambao maombi yao ya hifadhi yanakataliwa, kama vile Anis Amri. Je wawekwe katika vituo vya wanaosubiri kufukuzwa, au hata kizuizini ikiwa wanachukuliwa kuwa wenye hatari? Na ni nchi gani zichukuliwe kuwa salama kuweza kuwarejesha huko waomba hifadhi waliokataliwa?

Zaidi ya hayo, yapo mambo ambayo inabidi yafanyike.Ujerumani haipaswi kuwavumilia wahubiri wa chuki wanaotumia vyumba vya nyuma misikitini, na kuna sheria inayoruhusu kufanya hivyo, na nchi za Ulaya zinapaswa kushirikiana zaidi, kuhakikisha kwamba watu hatari hawalikwepi jicho la vyombo husika.

Maswali mengine yatajitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi. Wanasiasa ambao hawatatoa majibu sahihi, watakuwa hawatilii maanani wasiwasi wa raia kwa uzito unaohitajika.

 

Mwandishi: Fabian von der Mark

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Yusra Buwayhid

http://www.dw.com/en/opinion-the-debate-on-national-security-is-open/a-37006024