1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Wamisri hawana cha kuchagua

27 Mei 2014

Mwaka mzima baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Misri, raia wanamchagua mkuu mpya wa taifa hilo kubwa la Kiarabu, lakini Louay Mudhoon wa Idhaa ya Kiarabu ya DW anasema hiyo haimaanishi demokrasia.

https://p.dw.com/p/1C7Or
Loay Mudhoon wa Idara ya Utamaduni ya Deutsche Welle.
Loay Mudhoon wa Idara ya Utamaduni ya Deutsche Welle.Picha: DW

Kama zilivyokuwa chaguzi za zama za Hosni Mubarak, ndivyo ulivyo uchaguzi huu. Kimsingi tayari matokeo yameshapangwa kwa ajili ya kumtangaza mkuu wa zamani wa jeshi, Abdelfattah al-Sisi ameshinda kwa kishindo. Hata Wamisri waishio nje ambao waliopiga kura zao mwanzoni, al-Sisi alipata asimilia 94 ya kura zao.

Mtu anaweza kudhani kuwa hayo ni matokeo yaliyovunja rikodi, lakini kwa kuzingatia hali ya mambo katika miezi ya hivi karibuni nchini Misri, hakuna la ajabu hapo.

Baada ya kuangushwa kwa Mohamed Mursi mwezi Julai 2013, kilichoondoshwa hakikuwa kikundi cha Udugu wa Kiislamu tu, bali pia katiba ya nchi hiyo. Al-Sisi aliagiza kamisheni yake mwenyewe kuandika katiba mpya, ambayo pasi kuwa na uwakilishi wa wananchi, ilifuma katiba inayoyaweka mahitaji ya kijeshi kuwa ndio msingi wa demokrasia hiyo ya Mto Nile.

Hasara ya demokrasia

Kilichofuatia baada ya hapo wala hakikuhusiana kabisa na misingi ya demokrasia ya kiliberali iliyokuwa chimbuko la mapinduzi ya umma ya tarehe 25 Januari 2011. Sio tu kwamba kundi la Udugu wa Kiislamu lilianzishiwa kampeni ya kuchafuliwa jina na vyombo vya habari vya serikali, bali pia lilifanywa lionekane kuwa ni zimwi linalotishia usalama wa ndani wa nchi hiyo.

Hata makundi ya upinzani yenye mirengo kiliberali na isiyoelemea dini, hasa watetezi wa demokrasia na wanamapinduzi wa awali kabisa, wameteswa na kuuawa kinyama.

Wakati huo huo, mashirika ya haki za binaadamu yanaripoti kiwango kikubwa kabisa cha uvunjwaji wa haki za binaadamu na kuongezeka kwa mateso ya makusudi dhidi ya mahabusu na wafungwa nchini humo. Hii ni bila ya kutaja ile hukumu ya jumla jamala ya kifo iliyotolewa kwa mamia ya wafuasi wa Udugu wa Kiislamu.

Uchaguzi usio na kuchagua

Jumla ya mambo yote hayo yanasema kitu kimoja: nacho ni kwamba kwenye uchaguzi huu, Wamisri hawana uchaguzi. Hawana chaguo lililo makini, kwa sababu upinzani wa kweli ama umepigwa marufuku au umeufyata mkia.

Hamdeen Sabahi anaonekana kuwa yupo hapo kujenga taswira tu ya kuwa huu ulikuwa uchaguzi wa kidemokrasia, lakini hata yeye mwenyewe anajua kuwa njia ya kuelekea demokrasia ya Misri ni propaganda tupu.

Juu ya yote, al-Sisi sio mtumishi wa umma kama anavyopenda kujinasibisha. Huyu ni – na ataendelea kubakia kuwa – mtu wa jeshi. Ni jeshi ndilo linalomaanisha kila kitu Misri, limekuwa hivyo, na litabaki hivyo.

Ndilo linaloongoza takribani taasisi zote za kiserikali, kuanzia mahakama inayotumikia siasa za dola, hadi wizara ya mambo ya ndani inayofahamika kwa kukandamiza kwake upinzani, na mfumo mzima wa kimangimeza na propaganda inayoonekana kwenye vyombo vya habari vya umma.

Kituko ni kwamba, kundi ambalo linajifanya kufuata siasa za Kiislamu la Kisalafi limekuwa wafuasi wakuu wa kiongozi huyu mpya wa Misri. Ama ikiwa linafanya hivyo kwa kupapia maslahi yake au shinikizo la Saudi Arabia tu, hilo litafahamika baadaye.

Mwandishi: Loay Mudhoon/DW HGD Global
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga