1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Wimbi la siasa za kizalendo lazimwa

16 Machi 2017

Lengo limetimia. Hakuna tsunami ya kisiasa iliyotokea katika uchaguzi wa Uholanzi. Nchi hiyo imeonyesha wanasiasa wa siasa kali za kizalendo wanaweza kuzuiwa. Mwandishi wa DW Bernd Riegert anasema Ulaya sharti ijifunze.

https://p.dw.com/p/2ZHME
Niederlande Mark Rutte und Geert Wilders in Den Haag
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Nijhuis

Wafuasi wa dhati wa vyama vya kidemokrasia nchini Ufaransa, Ujerumani na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya sasa wanaweza kupumua. Uholanzi haitumbukii katika mkondo wa siasa kali za kizalendo. Waziri mkuu wa siasa za kiliberali anabakia madarakani huku mwanasiasa anayetilia shaka Umoja wa Ulaya na anayeeneza chuki dhidi ya uislamu, Geert Wilders, hakosi hofu au matumaini, kulingana na maoni ya mtu binafasi.

Kufuatia ushindi wa wafuasi wa siasa za kizalendo nchini Uingereza kupitia kura ya maoni ya kuiondoa nchi hiyo kutoka kwa Umoja wa Ulaya, Brexit, na matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Marekani, wapiga kura wametuma ujumbe wa wazi kabisa: mchezo unaishia hapa. Raia wa Austria pia, kwa kiwango kidogo cha kura, walimzuia mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia kuwa rais, ingawa ofisi yake kwa kiwango kikubwa ni ya uwakilishi tu.

Uholanzi ni ishara kwa chaguzi za Ufaransa na Ujerumani

Uchaguzi wa Uholanzi yumkini ukawa na athari kubwa muhimu katika uchaguzi wa urais nchini Ufaransa mnamo mwezi Mei mwaka huu na uchaguzi wa bunge nchini Ujerumani mwezi Septemba. Ujumbe ukiwa kwamba wafuasi wa siasa kali za kizalendo wanaweza kuzuiwa.

Wapiga kura wa Uholanzi yaonekana hawakumuamini Geert Wilders kuwa na uwezo wa kuongoza vyema au kuushughulikia barabara mgogoro na Uturuki, kama kwa njia fulani angekuwa katika nafasi ya kupitisha maamuzi. Mipango yake kwa matatizo yanayoikabili Uholanzi ilidhirika haikupikwa ikaiva, sawa na jinsi tunavyoshuhudia nchini Marekani na Uingereza.

Kaulimbiu si suluhisho

Wafanya kampeni za kisiasa nchini Ufaransa na Ujerumani lazima sasa watangaze wazi kwamba wafuasi wa siasa kali za kizalendo hawana chochote cha kutoa mbali na kaulimbiu. Hata hivyo, tatizo nchini Ufaransa ni kwamba mgombea wa tabaka la kati, Francois Fillon, anajichimbia kaburi lake mwenyewe. Mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen sasa ana mshindani mmoja tu ambaye ni kitisho kwake. Kama Wafaransa wanataka kumzuia Le Pen, watalazimika kumchagua mgombea huru kijana Emmanuel Macron.

Riegert Bernd Kommentarbild App
Mwandishi wa DW, Bernd Riegert

Ujerumani inakabiliwa na hali tofauti. Akiimarishwa na matokeo ya uchaguzi wa Uholanzi na hoja za msingi, kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na watu wengine wenye madaraka ya kisiasa wanaweza kutimiza kile kinachoonekana hakiwezekani - kukifanya chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD, kuwa kidogo kabisa kadri iwezekanyavyo.

Mabadiliko ya kisiasa

Hata kuwadhibiti wafuasi wa siasa kali za kizalendo kumekuja na gharama zake. Angalau nchini Uholanzi chama cha kiliberali cha waziri mkuu, Mark Rutte, VVD, kimeegemea mrengo wa kulia. Kilitoa kauli zaidi za kizalendo ili kuuzima upepo mkali wa Geert Wilders uliokuwa ukivuma sana.

Wanasiasa wa kizalendo huenda hawakushinda, lakini bado wanashawishi ajenda ya kisiasa na mienendo ya vyama vya kihafidhina katika mataifa jirani pamoja na nguvu ya vyama vya kiliberali katika ulingo wa siasa.

Chonde chonde Umoja wa Ulaya

Kwa Umoja wa Ulaya, uchaguzi wa Uholanzi una maana umoja huo hautakiwi kukaa tu na kukodoa macho. Badala yake unatakiwa utumie kasi hii mpya iliyojitokeza nchini Uholanzi. Katika mkutano wa kilele wa umoja huo utakaofanyika mjini Roma, Italia, wiki ijayo, viongozi wa Ulaya sharti watoe jawabu la pamoja kwa hali ya kukatisha tamaa na mienendo ya kizalendo. Matokeo hasi nchini Hungary na Poland, bila kusahau serikali ya kizalendo ya siasa za mrengo wa kushoto ya Ugiriki, lazima yapingwe na yakataliwe.

Wapiga kura wa Uholanzi wamelizuia wimbi la siasa kali za kizalendo. Sasa Umoja wa Ulaya unahitaji kujenga nyenzo zaidi za kulizuia wimbi hilo lisienee.

Mwandishi: Roegert, Bernd
Tafsiri: Josephat Charo
Mhariri: Saumu Yusuf