1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya Andreas Noll

17 Novemba 2006

Jee Ufaransa ipo njiani kupata rais wa kwanza mwanamke katika historia yake? Hayo yameanza kuonekana baada ya mwanasiasa wa chama cha kisoshalisti bibi Segolene Royal kuchaguliwa na chama hicho kugombea urais mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/CHL7

Mama huyo amechaguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura kukiwakilisha chama chake katika uchaguzi wa rais mwaka ujao nchini Ufaransa.Mama huyo mwenye umri wa miaka 53 aliwashinda wajumbe wengine, ikiwa pamoja na aliekuwa w aziri mkuu wa Ufaransa bwana Laurent Fabius .

Hakuna mtu alietarajia hapo awali kuwa angeliweza kuwashinda wapinzani wake katika raundi ya kwanza.

Kwa muda wote amekuwa juu katika kura za maoni. Na hata sasa wachunguzi wa maoni wanasema kuwa mwanamke huyo Segolene Royal anaweza kushinda katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka kesho nchini Ufaransa.

Na iwapo bibi Hilary Clinton atashinda katika uchaguzi wa rais nchini Marekani, basi itafarijika kuwaona wanawake watatu katika nyadhifa za juu yaani, Angela Merkel wa Ujerumani, Segolene Royal wa Ufaransa na Hilary Clinton wa Marekani.

Zipo sababu za kuamini kuwa bibi Royal anaweza kushinda.Na awali ya yote ni uwezo na uzoefu wake. Ana elimu ya juu.Alikuwa mshauri wa rais Francois Miterrand. Pia aliwahi kuwa waziri wa mazingira mwanzoni mwa miaka ya 90 na baadae waziri wa masuala ya familia.

Lakini anakabiliwa na changamoto ya kukileta chama chake pamoja ambacho sasa kimegawanyika. Chama cha kisoshalisti nchini Ufaransa kimo katika hali ya kubabaika-kwani hakijui wapi kisimame.

Jee mwanamke huyo atafanya nini mbele ya washindani wake wanaojitambua wenyewe kuwa masoshalisti wa mlengo wa kushoto kabisa ndani ya chama chake ? Segolene Royal anasema kuwa yeye ni mwanasiasa mwenye falsafa ya kutambua hali halisi.

Lakini anapaswa kutambua kwamba sasa changamoto kubwa zaidi ndio inaanza. Amepita kwa urahisi katika kinyang’anyiro cha ndani ya chama chake.

Lakini anapaswa kuruka kihunzi kingine kirefu-Nicolas Sarkozy mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa ambae sasa ni waziri wa mambo ya ndani nchini Ufaransa.Yeye pia atagombea urais na anajua namna ya kutumia vyombo vya habari. Yeye pia ana lengo la kumaliza miaka 12 ya urais wa bwana Chirac.

Chirac bado anafikiria kugombea kwa mara ya tatu.

Bibi Segolene Royal ni mwanasiasa maarufu. Kwa mujibu wa kura za maoni mwanamke huyo anaweza kumshinda bwana Sarkozy katika uchaguzi wa mwaka kesho.

Kiwango cha kura alichopata ndani ya chama chake kilichomwezesha kushinda katika raundi ya kwanza pamoja na kura za maoni ni msingi wa matumaini kwa mama huyo .